• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Maelfu wafurika Pwani usalama ukiimarishwa

Maelfu wafurika Pwani usalama ukiimarishwa

WINNIE ATIENO NA BRIAN OCHARO

SERIKALI imemwaga polisi wa kutosha katika maeneo hatari Pwani, huku mamia ya wasafiri kutoka mashambani wakimiminika kufurahia sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Kamanda wa Polisi Ukanda wa Pwani, Bw Manase Musyoka na Mshirikishi wa eneo hilo, Bw John Elungata, waliwahakikishia watalii wa ndani na wa nje na wenyeji kuwa hatua za kutosha za usalama zimewekwa kuhakikisha usalama wao.

‘Tuko tayari kwa sherehe hizo na tumetuma maafisa wa kutosha wa usalama ili kuimarisha usalama katika ufuo wa bahari, maeneo ya ibada na maeneo mengine maarufu ili kuhakikisha wakazi na wageni wanafurahia msimu huu wa likizo wenye amani na usalama,’ Elungata alisema wakati wa mahojiano na Shirika la Habari la Kenya Jumatatu katika ofisi yake ya Uhuru na Kazi huko Mombasa.

Bw Elungata ambaye alikuwa pamoja na Bw Musyoka aliuomba uongozi wa maeneo ya ibada na wananchi kwa ujumla kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa kuhusu mtu yeyote anayetuhumiwa au kufanya vitendo visivyo halali.

‘Wale wanaosimamia misikiti, makanisa na majengo mengine ya ibada wanapaswa kuanzisha uchunguzi na hatua zingine za usalama kwa ajili ya ulinzi,’ aliongeza Bw Musyoka .Wakati huo huo, Bw Elungata aliwasihi wapenda likizo kuzingatia kanuni zilizowekwa na Wizara ya Afya kudhibiti kuenea kwa virusi vya Covid-19.

Amesisitiza umuhimu wa kuheshimu kuweka umbali, kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni au sanitaiza na kuvaa barakoa katika maeneo ya umma.Aliwataka wenyeji na wageni kuepuka maeneo ya msongamano wa watu hasa kwenye fukwe, sehemu za burudani na vyombo vya usafiri wa umma.’

Wale watakaokiuka itifaki za Wizara ya Afya zinazolenga kupambana na kuenea kwa virusi vya corona watakamatwa na kufikishwa mahakamani,’ aliongeza Bw Elungata.Kwa upande wake, Kamanda Musyoka aliwakaribisha wageni wote Pwani na kuwahakikishia usalama wao wakati huu na baada ya msimu wa likizo.

Musyoka aliwataka wamiliki wa mabaa na maeneo mengine vya burudani kuhakikisha kuwa kuna ufuasi kamili wa itifaki za Covid-19 na kufunga maduka yao kulingana na leseni zao za utendakazi.Aliongeza kuwa polisi watashirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) katika utekelezaji wa kanuni za trafiki akisema magari ya utumishi wa umma na madereva wanapaswa kuepuka kuendesha gari kizembe wakati wa sikukuu.

Licha ya janga la Covid-19, maelfu ya wageni wa ndani na nje ya nchi wanakusanyika katika hoteli mbalimbali, vyumba na vituo vingine vya watalii huko Mombasa na maeneo mengine ya pwani wakati wa msimu huu wa likizo.Ukaguzi uligundua kuwa hoteli nyingi zimeweka hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi ili kuhakikisha ufuasi kamili wa itifaki za Covid kama ilivyoainishwa na Wizara ya Afya.

Wamiliki wa hoteli na wale walio katika biashara zinazohusiana na utalii wana matumaini kuwa kupata faida msimu huu na wanatarajia kupata wageni wengi ikilinganishwa na mwaka jana kufuatia ongezeko la watu ambao wanaomba kuhifadhiwa nafasi katika hoteli hizo huku wengine wakipiga simu kuulizia nafasi hizo.

Sekta ya utalii iliteseka zaidi wakati sheria za kudhibiti maambukizi ya Covid-19 viliwekwa kwani ilipelekea kupungua kwa kiasi kikubwa idadi ya watalii hivyo kuchangia kwa sekta hiyo kuenda chini.’Hoteli katika eneo hili zinapokea maombi ya kuhifadhi nafasi ambayo inatutia moyo huku wale wanaokuja likizoni nchini wakichukua asilimia kubwa zaidi,’ Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli (Pwani) Sam Ikwaye alisema

.Ikwaye alisema hoteli na wadau wengine wanatarajia msimu mzuri wa likizo ikilinganishwa na mwaka jana ambapo sekta hiyo ilipata pigo kubwa kufuatia kufungwa na vikwazo vingine ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya korona.’Janga hili la kimataifa iliathiri vibaya sekta ya hoteli na kulazimisha taasisi nyingi kufunga au kupunguza wafanyikazi wao,’ akaongeza.

Aidha, alibaini kuwa kuondolewa kwa kafyu imeleta afueni kubwa kwa sekta za hoteli na burudani lakini akatoa wito kwa wahusika wote katika sekta hiyo kutekeleza kwa uthabiti itifaki zote za afya wakati wa sherehe hizo.

You can share this post!

Ushindani mkali Team Kenya nusra umfanye awakimbilie Bahrain

Mgomo wanukia ligini EPL

T L