• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Maina Njenga ‘atekwa nyara’

Maina Njenga ‘atekwa nyara’

NA MERCY KOSKEI

ALIYEKUWA kiongozi wa kundi haramu la Mungiki, Bw Maina Njenga na msaidizi wake Felix Lakishe wanasemekana kutekwa nyara na watu wasiojulikana Jumamosi usiku, Septemba 16,2023 katika Kaunti ya Kiambu.

Akithibitisha utekaji nyara huo, wakili wake Ndegwa Njiru ameambia Taifa Leo Dijitali kuwa kisa hicho kilitokea saa tano usiku katika eneo la Banana, Kaunti ya Kiambu.

Kulingana naye, mteja wake alizuru shamba lake katika Kaunti ya Laikipia siku ya Jumamosi ambapo alishinda siku mzima kabla kuelekea Kiambu kwa ajili ya mkutano wa kifamilia.

Hata hivyo, akiwa njiani alipitia nyumbani kwa rafiki yake eneo la Banana.

Watu wasiojulikana walifika na kutaka wazungumze naye.

Kulingana na wakili Ndegwa, walivuta mteja wake na kumweka ndani ya gari  lililokuwa na nambari ya usajili ya Sudan na kuondoka pamoja na msaidizi wake.

Bw Njiru alisema kuwa watu hao hawakujitambulisha wala kumpa sababu za kumkamata, akisema “waliwateka nyara na kuwapeleka eneo lisilojulikana”.

“Njenga alinipigia simu pamoja na familia yake na kutufahamisha kuwa alikuwa anapelekwa katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI), lakini baadaye walimpokonya simu na kuizima. Kwa sasa hatuna habari zozote kuwahusu,” alisema wakili huyo.

Kulingana na Bw Njiru, huenda watafikishwa katika Mahakama ya Makadara Jumatatu, Septemba 18, 2023 kwa ajili ya kutajwa kwa kesi inayomkabili Bw Njenga.

“Hatujui ni kwa nini wamemteka nyara. Wanatafuta sababu ya kumkamata asipofika mahakamani. Kinachoshangaza ni kuwa maafisa wa polisi hawajazungumzia kuhusu tukio hilo,” alisema.

Mei 2023, iliripotiwa kuwa polisi walivamia nyumba tatu za Njenga katika kaunti za Nairobi, Nakuru, na Laikipia.

 

  • Tags

You can share this post!

Samidoh adai alitaka kuwa wakili, akifichua alama zake za...

Alfred Keter: Tuonyeshwe vituo vya petroli vya Kenya Kwanza...

T L