• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:21 PM
Alfred Keter: Tuonyeshwe vituo vya petroli vya Kenya Kwanza na Azimio

Alfred Keter: Tuonyeshwe vituo vya petroli vya Kenya Kwanza na Azimio

NA SAMMY WAWERU

ALIYEKUWA mbunge wa Nandi Hills, Alfred Keter ameikashifu vikali serikali ya Kenya Kwanza kufuatia nyongeza ya bei ya mafuta ya petroli.

Akionekana kumshambulia Rais William Ruto, mwanasiasa huyo mkakamavu amesema wanaoendelea kuumia zaidi kutokana na mfumko wa bei ya mafuta ni wananchi wa mapato ya chini.

Ongezeko la mafuta ya petroli, limesababisha bei ya bidhaa za kimsingi kuwa ghali na gharama ya maisha kupanda mara dufu.

“Mkiongezea bei ya mafuta, mnatesa wale wa chini kuliko matajiri,” Bw Keter akasema.

Kupitia video inayosambaa mitandaoni, mwanasiasa huyo anaskika akiisuta serikali ya Dkt Ruto akiitaka kutangaza vituo vya petroli vya Kenya Kwanza na Azimio – Upinzani.

“Mtuonyeshe vituo vya mafuta vya serikali na vya upinzani,” alisema.

Matamshi hayo yanaashiria kulenga kauli ya Waziri wa Biashara, Moses Kuria ambaye majuzi kupitia mahojiano na runinga ya Citizen alidai kuwa gharama ya maisha chini ya Kenya Kwanza imepungua ikilinganishwa na wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, ambaye kwa sasa amestaafu.

Katika kile kilionekana kama kupotosha umma, Bw Kuria alisema kwamba baadhi ya maeneo nchini bei ya bidhaa ni nafuu ikilinganishwa na mengine.

Maisha yanaendelea kuwa magumu zaidi nchini hasa baada ya bei ya bidhaa za petroli kupanda kwa kiwango kikubwa zaidi katika historia ya taifa hili.

Bei ya petroli ilipanda kwa Sh16.9 kwa lita. Nayo dizeli ikaenda juu kwa Sh21.31 huku bei ya mafuta taa ikipaa kwa Sh33.32 kwa lita moja.

Petroli sasa inauzwa Sh211.64 kwa lita jijini Nairobi huku dizeli ikiuzwa kwa Sh200.9 kwa lita, nayo mafuta taa yakiuzwa kwa Sh202.6 kwa lita.

Bei hiyo ilitangazwa mnamo Septemba 14, 2023 na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Petroli (EPRA).

  • Tags

You can share this post!

Maina Njenga ‘atekwa nyara’

Viboko wahangaisha wakazi na wavuvi Naivasha wakivamia...

T L