• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Maisha ya kijijini ni matamu – Gachagua

Maisha ya kijijini ni matamu – Gachagua

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amesema “unaweza ukamtoa mtu kijijini lakini hilo halitafuta kumbukumbu nzuri za maisha ya kijijini”.

Amesema hayo baada ya kufanya mazoezi ya kutembea ambapo pia amepata fursa ya kukutana na kutangamana na wakazi wa Mlima Kenya wakiendelea na shughuli zao za kutafuta riziki na kujenga uchumi wa nchi.

“Kila mara nikiwa kijini ninapenda sana kufanya mazoezi ya kutembea huku pia nikipiga stori na raia – kwa kweli huwa ninacheka nao pamoja tukitaniana,” amesema Bw Gachagua.

Naibu Rais Rigathi Gachagua (kushoto) akionja maisha ya kijijini. Amesema akiwa huko vijijini hufurahia maisha na kukumbuka maisha yake ya utotoni. PICHA | HISANI

Kwenye ziara hiyo amepata fursa ya kipekee kumtembelea Peris Gathoni ambaye alikuwa rafiki wa kufa kuzikana na marehemu mama yake Bi Martha Kirigo.

“Wawili hao ni wanawake jasiri waliojitolea kutulea,” Naibu Rais ametoa sifa kumrejelea mamake na Bi Gathoni.

Vile vile Naibu Rais amekutana na wanafunzi wa shule za msingi na za upili wakielekea shuleni.

“Kukutana na wanafunzi kumenikumbusha jinsi nilivyokuwa nikienda katika Shule ya Msingi ya Kabiru-ini kila alfajiri miguu peku bila vyatu bila ya kujali umande na baridi kali.

Naibu Rais Rigathi Gachagua akipiga stori na na muuzaji wa maziwa. PICHA | HISANI

Njiani amekutana na muuzaji wa maziwa na hapo wakazungumza japo kwa kifupi.

“Nimemhakikishia mfugaji huyo anayeuza maziwa kwamba serikali inalenga kuimarisha sekta hiyo na wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wataanza kupata pesa za kuwafaa,” amesema Bw Gachagua akisema wakazi wengi wa eneo la Mlima Kenya wanafurahia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya Kenya Kwanza ikiongozwa na Rais William Ruto.

Naibu Rais Rigathi Gachagua (wa pili mbele kulia) akiwa kwenye mazoezi ya matembezi katika eneo la Mlima Kenya mnamo Agosti 9, 2023. PICHA | HISANI

Rais Ruto anakamilisha ziara ya siku tano eneo la Mlima Kenya kwa kuzuru Naromoru, Kaunti ya Nyeri, kabla ya kuelekea Gichugu katika Kaunti ya Kirinyaga na kisha Thika katika Kaunti ya Kiambu.

Naibu Rais akitaniana na mwanakijiji huku wakiangua kicheko. PICHA | HISANI
  • Tags

You can share this post!

Koome ahamisha jaji aliyepiga breki Sheria ya Fedha ya 2023

Mtu mmoja afariki baada ya lori kuvuruga nyaya za umeme

T L