• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Koome ahamisha jaji aliyepiga breki Sheria ya Fedha ya 2023

Koome ahamisha jaji aliyepiga breki Sheria ya Fedha ya 2023

NA SAM KIPLAGAT

JAJI Mugure Thande aliyesimamisha utekelezaji wa Sheria ya Fedha 2023, ni kati ya majaji waliohamishwa Jumanne na Jaji Mkuu Martha Koome.

Bi Thande aliondolewa kutoka Mahakama ya Masuala ya Sheria, na sasa atakuwa Jaji wa Mahakama ya Malindi.

Kwenye tangazo la Jaji Msimamizi wa Mahakama Kuu Eric Ogolla, majaji wengine waliohamishwa ni; David Majanja aliyeteuliwa kuongoza kikosi cha majaji watatu wa kusikiza kesi hiyo ya Sheria ya Fedha, iliyowasilishwa na Seneta wa Busia, Okiya Omtatah.

Pia kuna Jaji Hedwig Ong’udi ambaye ameondolewa kutoka Mahakama ya Sheria na Haki za Binadamu hadi Mahakama Kuu ya Nakuru.

Jaji Hillary Chemitei ametolewa Nakuru hadi Milimani, Nairobi katika Mahakama ya masuala ya Familia.

Jaji Maureen Odero ameondolewa kutoka mahakama hiyo ya Familia na sasa atakuwa Jaji wa Nyeroi kuchukua nafasi ya Jaji Florence Muchemi aliyepelekwa Thika.

Jaji Chacha Mwita ameondolewa Milimani kutoka Mahakama inayoshughulikia Biashara na Ushuru na kuchukua nafasi ya Jaji Ong’udi katika Mahakama ya Sheria na Haki za Binadamu.

Jaji Diana Kavedza ameondolewa Milimani kwenye Mahakama ya kushughulikia Uhalifu na atahudumu katika mahakama za Kibera na Kahawa.

Jaji Patricia Gichohi amehamishwa kutoka Kisii hadi Nakuru na kubadilishana na Jaji Teresa Odera.

Jaji Peter Mulwa ameondolewa Kiambu na atachukua nafasi ya Jaji Mwita iliyoko Milimani, Nairobi.

Wengine ni Jaji Aleem Visram aliyehamishwa kutoka Mahakama ya Masuala ya Raia hadi ile ya Masuala ya Biashara. Na jaji wa mwisho kuhamishwa ni Lilian Mutende atakayekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mahakama ya Utoaji Huduma.

Jaji Thande anatambuliwa kwa kuzima utekelezaji wa Sheria ya Fedha 2023, kwa kurefusha marufuku hadi Julai 10, kabla majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa kuiruhusu serikali ianze kutekeleza sheria hiyo.

Waziri wa Fedha Prof Njuguna Ndung’u alikuwa amedai mbele ya majaji hao wa Rufaa kwamba kusimamishwa kwa utekelezaji wa sheria hiyo kuliathiri ukusanyaji mapato.

“Nataka kuwafahamisha kwamba Mheshimiwa Jaji Mkuu amefanya mabadiliko katika idara ya Mahakama, yatakayoanza kutekelezwa kuanzia Oktoba 2,” ilisema taarifa aliyoitangaza jaji Ogolla.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali, Azimio wajue hatima ya nchi ni kwao

Maisha ya kijijini ni matamu – Gachagua

T L