• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Maseneta waelezwa sababu ya neti hafifu kuingizwa nchini

Maseneta waelezwa sababu ya neti hafifu kuingizwa nchini

NA MARY WANGARI

UKOSEFU wa ufadhili wa kutosha kutoka kwa serikali ulisababisha shirika la Global Fund kununua neti ambazo hazina dawa kali ya kuzuia mbu wanaobeba viini vinavyosababisha malaria.

Seneti ilielezwa katika kikao Jumanne kwamba Global Fund haikununua vyandarua vya kisasa ambavyo vimeongezwa kemikali ya PBO yenye uwezo wa kuua aina mpya ya mbu.

Global Fund ilinunua vyandarua vya zamani aina ya pyrethroids badala ya aina ya kisasa ya PBO ambayo imependekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutumika katika maeneo yenye makali ya malaria.

Kamati ya Seneti kuhusu Afya vilevile ilisikia kuwa Global Fund ililazimika kusaka fedha za ziada ili kufanikisha ununuzi wa vyandarua.

Waundasheria wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago, waliitaka Global Fund kufafanua ni kwa nini ilinunulia Kenya vyandarua vilivyopitwa na wakati ilihali shirika hilo hununulia taifa jirani la Uganda vyandarua vya kisasa.

“Mbona Global Fund hununulia Uganda PBO LLINs na ilipofikia Kenya wakuu waliamua kununua Pyrethroid LLINs ilhali tunashiriki mpaka ambapo maambukizi ya malaria yamekithiri eneo hilo?” alihoji Seneta Mandago.

Kupitia mwakilishi wake, Kampuni ya PricewaterhouseCoopers, Global Fund ilikiri kununua aina tofauti ya vyandarua kwa maeneo tofauti ikijikita kwenye viambajengo viwili vikuu.

“Global Fund hununua vyandarua tofauti katika maeneo tofauti. Kuna masuala muhimu yanayotuelekeza katika mchakato wa ununuzi ikiwemo kuwepo raslimali za kutosha na kuhakikisha wanajamii wote lengwa wananufaika,” alisema Mkurugenzi wa PwC, Jospeh Kagiri.

“Ni sharti tungehakikisha wanajamii wote wamenufaika. Ufadhili wa serikali ya Kenya haukutosha na hata tulilazimika kusaka hela za ziada.”

Mawasilisho ya Kemsa mbele ya Seneti yaliashirika kuwa Wizara ya Afya iliandikia barua Mamlaka ya Kusambaza Vifaa vya Matibabu Nchini (Kemsa) mnamo Februari 21, 2023, ikisema aina ya neti zilizopangiwa kununuliwa ilitofautiana na zilizoitishwa.

Kulingana na ripoti iliyowasilishwa Seneti, Hazina Kuu ilijibu Kemsa kupitia barua mnamo Februari 24, 2023 ikisema aina ya vyandarua isibadilishwe, kwa kuwa iliashiria kisahihi nia ya kununua neti zisizo na PBO.”

“Tulichukua uamuzi huo kwa sababu vyandarua vya pyrethroid ni vya bei nafuu zaidi kuliko vyandarua vya PBO na ikizingatiwa hatukuwa na muda wa kununua idadi yote ya vyandarua vilivyohitajika. Wadau kutoka Hazina Kuu, Mpango wa Malaria na Global Fund waliafikiana kuwa hatua bora ilikuwa kutumia kikamilifu idadi ya vyandarua ambavyo tungeweza kununua kupitia ufadhili tuliopatiwa,” ilisema ripoti ya PwC.

Zaidi ya vyandarua 2 bilioni vilivyotiwa Dawa ya Kuangamiza Wadudu (ITN) vya kuzuia malaria vimesambazwa kote duniani kwa karibu miongo miwili tangu 2005, kwa mujibu wa WHO.

Awali, vyandarua vyote vilikuwa vikitibiwa kwa kutumia aina moja tu ya kemikali – pyrethroids.

Kadri miaka ilivyosonga, palikuwa na haja ya kutibu vyandarua na viungo vinginevyo vyenye makali ili kupambana na malaria huku mbu katika maeneo yenye viwango vya juu vya maambukizi wakizidi kuwa sugu.

Mnamo 2017 WHO ilianza kupendekeza aina mpya ya vyandarua inayojumuisha kemikali mbili – pyrethroids na PBO.

  • Tags

You can share this post!

Msimu wa 2022-23 Ligi ya Divisheni ya Kwanza wanawake...

‘Azimio wanajichekelea kuwatembelea majeruhi’

T L