• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Masharti makali ya Azimio kwa Kenya Kwanza

Masharti makali ya Azimio kwa Kenya Kwanza

NA WANDERI KAMAU

MIRENGO ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja bado inaendelea kupimana nguvu kuhusu duru ya pili ya Mazungumzo ya Maridhiano, inayotarajiwa kuanza upya, baada ya duru ya kwanza kusambaratika.

Misimamo hiyo inajitokeza licha ya pande hizo mbili kuwateua watu watakaoziwakilisha kwenye mazungumzo hayo.
Mnamo Jumatano, mrengo wa Kenya Kwanza, unaomwakilisha Rais William Ruto, uliwateua wawakilishi watano, siku moja baada ya Azimio kufanya hivyo.

Kenya Kwanza iliwateua Viongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na Seneti mtawalia-Kimani Ichung’wa na Seneta Aaron Cheruiyot (Kericho), Gavana Cecily Mbarire (Embu), Hassan Omar (Bunge la Afrika Mashariki -EALA) na Mwakilishi wa Kike Catherine Wambilianga (Bungoma).

Azimio, kwa upande wake, itawakilishwa na Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi, mbunge Amina Mnyazi (Malindi) na Seneta Okong’o Omogeni (Nyamira).

Licha ya mirengo hiyo kutangaza wawakilishi wake, Azimio imetoa masharti makali, ikisisitiza kuwa lazima yazingatiwe, ili mazungumzo hayo yaanze.

Azimio inasisitiza kuwa lazima mazungumzo hayo yaanze Jumatatu wiki ijayo.

Tayari, Bw Musyoka, ambaye ndiye kiongozi wa ujumbe wa Azimio, amemwandikia barua Bw Ichung’wa, akisisitiza kuwa muda utakuwa zingatio muhimu kwenye mazungumzo hayo.

Kwenye barua hiyo, Bw Musyoka anapendekeza mkutano wa kwanza wa jpande hizo mbili ufanyike katika Hoteli ya Serena, jijini Nairobi, hapo Jumatatu.

“Kutokana na uzito wa masuala tunayojadili, shauku ya watu wetu na hitaji la haraka kusuluhisha changamoto zinazolikabili taifa letu. Tunatoa mwaliko kwa ujumbe wa Kenya Kwanza katika Mazungumzo ya Maridhiano, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na kiongozi wa ujumbe huo katika mkutano wa kwanza utakaofanyika Serena, Nairobi, Jumatatu, Agosti 7, 2023, saa tano asubuhi,” akasema Bw Musyoka kwenye barua hiyo.

Sharti la pili ambalo Azimio imetoa ni kuwa lazima mazungumzo hayo yafanyike kwa muda wa mwezi mmoja.

Azimio inasisitiza kuwa lazima mazungumzo hayo yafanyike na kukamilika kati ya Agosti 1 na Agosti 31.

Inasema kuwa sababu ya kutoa sharti hilo ni “unafiki uliodhihirishwa na Kenya Kwanza” kwenye duru ya kwanza ya mazungumzo hayo.

“Ukosefu wa nia safi kutoka kwa Kenya Kwanza ndio chanzo kikuu cha kuvurugika kwa awamu ya kwanza ya mazungumzo haya. Lengo letu kuweka muda maalum ni kuhakikisha kuwa kila upande umepewa nafasi ya kutosha kujitayarisha bila kutoa visingizio vyovyote,” akasema aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Peter Munya, katika kikao na wanahabari wiki iliyopita.

Tatu, Azimio inasisitiza lazima suala gharama ya juu ya maisha lijumuishwe kwenye mazungumzo hayo, ikitaja hilo kuwa “suala kuu linalowatatiza Wakenya wengi kwa sasa”.

“Litakuwa kosa kubwa tukikosa kujadili gharama ya maisha. Hili ndilo suala lililotusukuma kuanza mazungumzo na wananchi,” akasisitiza Bw Musyoka.

Hata hivyo, Rais Ruto alisisitiza kuwa suala hilo halitakuwa katika ajenda za mazungumzo, kwani tayari, serikali ya Kenya Kwanza ina mpango kabambe wa kushughulikia suala hilo kupitia manifesto yake.

“Hatutakubali mtu yeyote kutuambia vile tutapunguza gharama ya maisha. Tushaanza juhudi hizo kupitia kwa utekelezaji wa manifesto yetu, kwa mfano, kupitia kuwapunguzia wakulima bei ya mbolea,” akasema Rais Ruto Jumatano.

MADAI YA ICHUNG’WAH

Azimio pia imesisitiza kuwa lazima isipewe masharti kuhusu masuala inayofaa kuwasilisha na yale ambayo haipaswi kuwasilisha kwenye vikao hivyo.

Hilo linafuatia taarifa iliyotolewa na Bw Ichung’wa wiki jana, ambapo alidai waliitoa pamoja na Bw Wandayi, ambaye ndiye Kiongozi wa Wachache katika Bunge.

Baadaye, Azimio iliipuuza taarifa ya Bw Ichung’wa, ikidai alijumuisha masuala ambayo haijakubali kuyawasilisha.

“Sisi hatutaiwekea masharti Kenya Kwanza kuhusu yale itakayowasilisha. Vivyo hivyo, haipaswi kutuwekea masharti,” ikaeleza Azimio kwenye kikao cha pamoja na wanahabari.

Tano, Azimio imeshikilia kuwa lazima mazungumzo hayo yaongozwe na aliyekuwa Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, kama mpatanishi kutoka nje.

Kulingana na Bw Munya, pendekezo hilo pia linatokana na “ukosefu wa nia safi” kutoka kwa Kenya Kwanza.

Hili ni licha ya baadhi ya wabunge wa Kenya Kwanza kusisitiza kuwa Bw Obasanjo anafaa “kushughulikia matatizo makubwa yanayoikumba Nigeria”.

Kauli hizo zilitolewa na wabunge watatu wa Kenya Kwanza- Nimrod Mbai (Kitui Mashariki), Clement Sloya (Sabatia) na Earnest Ogesi (Vihiga).

  • Tags

You can share this post!

Pasta ashtakiwa kujeruhi mwanamke nyeti akimuombea

JAGINA WA SPOTI: Alitikisa soka Harambee Starlets sasa ni...

T L