• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:50 AM
JAGINA WA SPOTI: Alitikisa soka Harambee Starlets sasa ni katibu FKF Pwani

JAGINA WA SPOTI: Alitikisa soka Harambee Starlets sasa ni katibu FKF Pwani

NA CHARLES ONGADI

NI kati ya wachezaji waliong’ara sana katika timu ya taifa ya akina dada ‘Harambee Starlets’ miaka ya 90 kabla ya kustaafu na kujitosa katika uongozi wa soka.

Lilian Nandudu,42, mlinzi wa zamani wa timu ya taifa ambaye kwa sasa ni Katibu wa Shirikisho la Soka Nchini kanda ya Pwani anayefanya kila njia kuinua hali ya soka kanda hilo.

Mbali na soka, Nandudu pia alikuwa mchezaji hodari wa Voliboli na Netiboli akiwa shule ya msingi ya Magongo chini ya mwalimu mkuu Ahaya Juma Ahaya.

“Nilijipata katika soka nikiwa na miaka saba pekee nikicheza na ndugu zangu wa kiume na baadaye timu ya wavulana ya Coolchester FC mtaani Bokole, Magongo, Kaunti ya Mombasa,” asema Nandudu.

Nandudu ambaye ni kitinda mimba katika familia ya watoto saba; wanne wa kiume na watatu wa kike anasema daima alijiunga na nduguze kila mara kucheza soka vichochoroni katika mtaa wa Bokole.

Ari hiyo ilimpelekea kujiunga na timu ya wavulana ya Coolchester na uhodari wake ulimvutia kocha wa timu hiyo aliyekuwa akimchezesha katika mechi zao za kirafiki.

Sifa zake zikaanza kusambaa kama moto mkali kwenye kichaka kikavu katika Kaunti ndogo cha Changamwe kutokana na ubora wake uwanjani.

“Hakukuwa na timu nyingi za wasichana kipindi hicho kwa hivyo nilikuwa nikipewa nafasi ya kuonesha weledi wangu wa kupepeta boli kwa mashabiki kabla mechi kuanza katika mechi iliyohusisha timu za wavulana,” asimulia Nandudu kwa furaha.

Timu ya soka ya akina dada ya CLS chini ya makocha Phylip Mwakio na Charles Kenga ilipoundwa, Nandudu alikuwa wachezaji wa kwanza kujiunga nayo.

Wakati CLS ilipobadilisha jina na kuwa Mombasa Railways Ladies FC, Nandudu alijumuika na wachezaji wenzake kama Ethel Wakesho, Akumu Migoya, Emmah Adar, Christine Nanjala, Amina Chitra, Grace Atieno miongoni mwa wengine.

Kikosi hiki kilichotetemesha soka Pwani na hata bara kikiwa chini ya mkufunzi Milucky Wanjala aliyehakikisha soka la akina dada Pwani inakuwa kwa kiwango kikubwa.

Nandudu aliitwa kwa mara ya kwanza katika timu ya taifa chini ya kocha Habil Nanjero na kuhudumu hadi alipoangika daluga zake mwaka wa 2005.

“Nilishuhudia changamoto kibao nikiwa katika timu ya taifa kipindi hicho, soka ya akinadada ilibezwa na viongozi na hamu ya kuleta mageuzi katika soka ikanichochea kujitosa katika uongozi wa Soka nchini,” afafanua mchezaji huyu wa zamani.

Aidha, anasema ukosefu nidhamu na kujituma miongoni mwa wachezaji umechangia wachezaji wengi kutodumu kwa kipindi kirefu huku akisema siri ya mafanikio katika soka ni nidhamu pekee.

  • Tags

You can share this post!

Masharti makali ya Azimio kwa Kenya Kwanza

Azimio kuwapa wafuasi mwelekeo Septemba

T L