• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 2:21 PM
Matiang’i ajibu madai ya wandani wa Dkt Ruto kuhusu maandalizi ya uchaguzi

Matiang’i ajibu madai ya wandani wa Dkt Ruto kuhusu maandalizi ya uchaguzi

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Usalama Fred Matiang’i amejitetea dhidi ya madai ya wandani wa Naibu Rais William Ruto kwamba yeye na mwenzake wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru wanaingilia utendakazi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa ajili ya kushawishi matokeo ya uchaguzi mkuu ujao.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Dkt Matiang’i alieleza kwamba wajibu wa wizara hizo mbili katika uchaguzi huo wa 2022 ni kuandaa mazingira bora ya kufanikisha shughuli hiyo.

“Sisi katika sekta ya usalama, huwa hatuendeshi uchaguzi—huo ni wajibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka na kazi yetu ni kuisadia tume hii kwa kutoa usalama,” akasema.

Dkt Matiang’i alisema kuwa shinikizo la wabunge wandani wa Dkt Ruto na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwamba yeye na Mucheru wanapaswa kujiuzulu wanalenga kumzuia kufanya kazi zao.

“Sijali na ukosoaji kutoka kwa wanasiasa kwa sababu lengo lao ni kuniharibia jina bila sababu yoyote,” akaongeza.

Mnamo Alhamisi wiki jana wabunge wandani wa Dkt Ruto, Ndindi Nyoro (Kiharu), Rigathi Gachagua (Mathira), Alice Wahome (Kandara) na Kimani Ichung’wa, walidai Dkt Matiang’i na Bw Mucheru wanapaswa kujiuzulu kwani wamegeuka “ajenti wa kiongozi wa ODM Raila Odinga”.

“Dkt Matiang’i na Bw Mucheru wameonyesha wazi kuwa wanampigia debe Raila Odinga. Kwa hivyo, hawafai kushiriki katika mchakato mzima wa maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao kwa sababu tayari wameonyesha wanampendelea. Waondolewe katika nyadhifa hizo au wahamishwe hadi wizara zingine,” akasema Bw Gachagua.

Wakiunga mkono kauli hiyo Mbw Nyoro, Ichung’wa na Bi Wahome walisema kuwa mawaziri hao wawili hawafai kushirikiana na IEBC katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Walisema hayo katika makazi rasmi ya Dkt Ruto katika mtaa wa Karen, Nairobi wakati ujumbe kutoka Murang’a na Kirinyaga ulimtembelea Naibu Rais.

Baadaye mnamo Ijumaa, Katibu Mkuu wa UDA Bi Veronica Kinyanjui aliiandikia IEBC barua akilalamikia kushirikishwa kwa Dkt Matiang’i na Bw Mucheru katika maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.

Mawaziri hao wawili pamoja na Jaji Mkuu Martha Koome ni miongoni mwa wadau walioshiriki katika mkutano ulioandaliwa na IEBC wiki jana kujadili mipango ya uchaguzi mkuu.

You can share this post!

Ruto ataka wapinzani waje na sera zao

Mahakama yaagiza Rotich ashtakiwe upya

T L