• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Cherargei ataka DCI na EACC zichunguze matumizi mabaya ya fedha za michezo

Cherargei ataka DCI na EACC zichunguze matumizi mabaya ya fedha za michezo

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Nandi Samson Cherargei anataka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuchunguza sakata ya matumizi mabaya ya Sh30 bilioni, fedha za Hazina ya Michezo Nchini.

Akiongea na wanabahari Jumanne katika majengo ya Bunge, Bw Cherargei alipendekeza kuwa maafisa wote wa mashirika ya michezo nchini na maafisa wa Wizara ya Michezo mchini akiwemo Waziri Amina Mohammed wachukuliwe hatua kali.

Seneta huyo aliwasuta maafisa wa Wizara ya Michezo kwa kuelekeza fedha nyingi za hazina hii kwa michezo ambayo sio maarufu badala ya fani kama vile Riadha, Kandanda, Ndondi na Voliboli ambazo hutengewa pesa kidogo mno.

“Kwa mfano, iweje kwamba michezo ambayo haina umaarufu sana nchini kama vile ‘Wood Ball Championship” itengewe Sh31 milioni na mchezo wa Kung Fu ambao ni maarufu nchini China utengewe Sh80 milioni ilihali michezo hii haina mashiko sana nchini? Mbona spoti maarufu kama vile Riadha, Kandanda, Ndondi na Mchezo wa Raga kunyimwa fedha?” akauliza Bw Cherargei.

“Inaonekana kuwa fedha hizi huelekezwa katika mifuko ya watu fulani, haswa maafisa katika Wizara ya Michezo. Hii ndiyo maana ninataka EACC na DCI iwachunguze maafisa hawa kwa lengo la kuwashtaki kwa kufuja pesa za umma,” akaongeza.

Bila kutoa ushahidi, Seneta Cherargei alidai jumla ya Sh23 bilioni kutoka Hazina hiyo ya Michezo zilitumika katika ujenzi wa viwanja vya michezo vya Kisumu, Wang’uru (Kirinyaga) na Kiringiti Kiambu lakini viwanja hivyo havijatimiza viwango vya kimataifa.

“Hii ni licha ya kwamba kiasi kukubwa cha pesa kilitumika katika ujenzi wa viwanja hivi,” akasema.

Bw Cherargei alisema kuwa tayari amewasilisha ushahidi wa kuonyesha jinsi fedha za Hazina hii zilivyotumiwa vibaya ili kusaidia EACC na DCI katika uchunguzi wao.

“Ikiwa asasi hizo hazitakamilisha uchunguzi kwa kipindi cha kati ya siku 14 na 21 basi sitakuwa na budi kufungua mashtaka dhidi ya wahusika katika sakata hii,” seneta Cherargei akatisha.

You can share this post!

Aguero kutochezeshwa na Barcelona kwa miezi mitatu ijayo...

USWAHILINI: Posa asili ya Kidigo ilivyofanikishwa kwa...

T L