• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
Mwanaharakati atozwa faini kwa kula hongo

Mwanaharakati atozwa faini kwa kula hongo

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA mshirikishi wa Kitaifa wa Bunge la Wananchi ametozwa faini ya Sh250, 000 ama atumikie kifungo cha miaka miwili gerezani akishindwa kuilipa.

Mahakama ya kuamua kesi za ufisadi katika Mahakama ya Milimani ilimpata Rodgers Mwololo na hatia ya kudai na kupokea hongo ya Sh150, 000 na Sh100, 000 mtawalia kutoka kwa Bw Lucas Munata Sameta.

Mwololo alishtakiwa kwamba mnamo Desemba 3, 2018 katika Hoteli ya Grand Quality, Nairobi akiwa mshirikishi wa Bunge la Wananchi aliitisha hongo ya Sh150, 000 lakini akapewa Sh100, 000 na Sameta.

Mwololo alishtakiwa chini ya kifungu cha sheria nambari 6(1) (a) cha kupambana na ulaji rushwa ya 2016.

Mshtakiwa huyo alitozwa faini ya Sh150, 000 kwa kudai hongo kiasi cha Sh150, 000.

Akishindwa kulipa faini hiyo atasukumwa jela miezi 12.

Kwa shtaka la tatu alitozwa faini ya Sh100, 000 ama atumikie kifungo cha mwaka mmoja jela.

Hata hivyo akipitisha hukumu hiyo hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Felix Kombo alimwachilia Mwololo kwa kosa la kudai mlungula wa Sh250, 000 kutoka kwa Sameta.

Mahakama ilisema mshtakiwa aliitisha hongo hiyo kusudi asitangaze katika vyombo vya habari madai kwamba kulikuwa dhuluma za kimapenzi zilizokuwa zimeshamiri katika hoteli hiyo.

 

  • Tags

You can share this post!

Leopards tayari kurarua Bandari Jumapili ugani Kasarani

Mmea wenye madini mengi kuliko vyakula vyote duniani

T L