• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mmea wenye madini mengi kuliko vyakula vyote duniani

Mmea wenye madini mengi kuliko vyakula vyote duniani

NA RICHARD MAOSI

Spirulina ni mmea wa rangi ya kijani kibichi ambao  mara nyingi hukua na kutapakaa juu ya maji, lakini sio watu wengi ambao wanafahamu kuwa wanaweza kuchuma riziki kutokana nao.

Isitoshe ni mmea ambao ni aina ya gugu maji , linaloweza kukuzwa ndani ya maji bila kutumia udongo na unafahamika kwa ukwasi mkubwa wa madini mwilini mwa binadamu..

Cha kustaajabisha ni kuwa mmea wenyewe unaweza kuvunwa kila baada ya siku mbili na hata siku moja, ambapo mkulima anapovuna huwa na unyevu.Akilimali ilizuru kijiji cha Sikali kaunti ya Kakamega ambapo tulikutana na Paul Nyongesa mkazi wa hapa akiendelea kuvuna mmea wa spirulina ili kuwauzia wateja wake.Nyongesa ni mkulima na mtaalam wa zao la spirulina ,Anaeleza kuwa ukianza kwenye makazi ya mtu binafsi ni zao ambalo linaweza kutumika kama chakula, pia ni lishe kwa wanyama ambao hufugwa katika boma.

“Mfano mzuri ni kama vile samaki ambao wakipewa spirulina hukua haraka na pia yale maji yake yanaweza kutumika kutengeneza mbolea,”akasema.

Anasema wakati wa kuvuna kichujio ndicho hutumika, na mkulima hushauriwa kuyasumbua maji kila wakati ili zao hili liweze kujitengeneza na kutoka hapo mkulima atakuwa na uwezo wa kuvuna kila siku kiwango cha gramu 10 katika kipimo cha kidimbwi cha mita moja mraba.

Inapovunwa hukaushwa na kusagwa kisha ikaongezwa kwenye vyakula vingine na kila bidhaa inayouziwa wateja huwa imeidhinishwa na shirika la Kenya Bureau of Standards.

Anasema maji ya kukuza spirulina hubadilishwa kila baada ya miezi sita na kutoka hapo mkulima anatakiwa kusafisha kidimbwi na kubadilisha maji, ili kuendeleza uzalishaji.

Alieleza kuwa spirulina ni bidhaa ambayo inakuzwa kwa kiwango cha juu katika mataifa ambayo huwa yamestawi kama vile Uchina na Japan.

Isitoshe alifichulia Akilimali kuwa ni wakulima wengi kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya ambao wamewekeza kwenye mradi wa kukuza spirulina katika hatua ya kufanikisha kilimo biashara.

Kulingana na Nyongesa ni mmea ambao unaweza kutumika kama dawa vilevile unaweza kutumika kama lishe na wakati mwingine unaweza ukakaushwa na kuuzwa kama unga.

Bw Nyongesa anasema kuwa katika kongamano la ulimwengu mnamo 1976 wanasayansi walifichua kwamba spirulina ndicho chakula bora kuliko vyakula vingine.

“Kwanza kina kiwango kikubwa cha madini ya protini na hakuna chakula kingine ambacho kinaweza kulinganishwa na zao hili,”akasema.

Aidha aliongezea kuwa spirulina huwa na vitamini E kwa wingi kushinda zao la parachichi ambalo linafahamika kwa madini haya.

Aidha madini ya Iron na calcium ni baadhi ya virutubishi muhimu ambavyo hupatikana kwenye zao hili ambalo, makundi mengi ya kijamii na ya ushirika kutoka mkoa wa Magharibi yameanza kuwekeza kwayo.

Nyongesa anaamini kuwa hiki ni chakula ambacho kinaweza kutumika katika mataifa yanayoendelea kupambana na maradhi yanayowakumba watoto na wazee, hususan ukosefu wa Kinga mwilini.

Katika maeneo ambayo kiwango cha shamba kinaendelea kupungua kutokana na ongezeko la idadi ya watu, kilimo hiki kinaweza kuwafaa wenyeji kwani jambo linalohitajika ni aina maalum ya chumba cha kivungulio(green house).

Isitoshe Paul Nyongesa amekuwa akiendesha mradi huu kwa ushirikiano na Chuo Kikuu Cha Masinde Muliro kwa ushirikiano na makundi ya akina mama na vijana ambao wanalenga kujiendeleza kimaisha.

Jambo la msingi katika ukuzaji wa aina hii ya zao ni upatikanaji wa eneo ambalo limejaa chembechembe za chumvi kwa wingi, pia inahitaji kiwango kikubwa cha joto na ndio maana imekuwa ikipandwa ndani ya chumba cha green house.

“Ni mmea ambao unaweza kufanya vyema kwenye joto ambalo sio la moja kwa moja kutoka kwa jua ndio maana niliamua kufunika mazao yangu, nikitumia aina spesheli ya karatasi,”akasema.

Isitoshe anasema kuwa mkulima atahitaji kuwa na mbolea ili kurutubisha maji yake ili yaweze kuwa na kiwango cha chumvi kinachohitajika.

Bila kusahau maji safi ambayo ndio hutumika kupanda spirulina, ambapo anawashauri wakulima ambao wanalenga kuanzisha aina hii ya kilimo kutafuta ujuzi wa wataalam kabla ya kuanzisha mradi wenyewe.

“Katika Chuo Kikuu Cha Masinde Muliro kuna wataalam wengi ambao wanajihusisha na taaluma hii ambayo inaaminika kuwa itawasaidia wakulima wengi mashinani , kujikwamua kutokana na hali ngumu ya kiuchumi,”anashauri.

Anasema kuwa ni mradi ambao ikiwa utakumbatiwa na vyama vya ushirika mijini na mashambani, itawasadia vijana kupigana na kero la ukosefu wa ajira.

Ikumbukwe kuwa spirulina inaweza kusaidia taifa kuokoa hela nyingi ambazo hutumika kuagiza mbolea za kigeni na hata madawa ya kutibu aina mbalimbali ya maradhi.

Nyongesa alieleza kuwa huu ni mmea ambao unaweza kuuziwa mashirika ambayo yanajali maslahi ya binadamu kama vile Umoja wa Kimataifa(UN) na kambi za wakimbizi kama vile Daadab.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Mwanaharakati atozwa faini kwa kula hongo

Serikali za kaunti kupokea Sh385 bilioni baada ya Rais...

T L