• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Mwanamume azama baharini baada ya kuokoa mwanamke na mtoto

Mwanamume azama baharini baada ya kuokoa mwanamke na mtoto

NA FARHIYA HUSSEIN

MWANAMUME mmoja amezama baharini alipokuwa akijaribu kumuokoa mwanamke wa umri wa miaka 45 katika Bahari Hindi.

Kilichokuwa kuwa kitendo cha kishujaa kiligeuka kuwa huzuni baada ya mwanamume huyo kutoweka kwenye ufuo wa Madubaha katika mji mkongwe wa Mombasa baada ya kusombwa na mawimbi makali.

Akithibitisha, Mkuu wa Kitengo cha Zimamoto na Majanga ya Dharura katika Kaunti hiyo Bw Ibrahim Basafar alisema mkasa ulitokea Ijumaa mwendo wa saa kumi jioni ambapo mwanamume huyo ambaye alikuwa akipunga upepo katika ufuo huo alimuona mwanamke huyo na msichana mdogo wakitapatapa baharini.

Bw Basafar alibainisha ya kwamba mwanaume huyo aliingia baharini na kufanikiwa kuwaokoa kwa usalama hadi kwenye ufuo wa bahari.

Lakini muda mchache baadaye, mwanamume huyo alipotea majini kwa njia isiyoeleweka, na mamlaka kwa sasa inaendelea na msako na uokoaji ili kumpata.

“Kwa bahati mbaya, mwanamke aliyekuwa na umri wa miaka 45 alifariki njiani akipelekwa hospitalini huku msichana akiwa katika hali mahututi katika Hospitali Kuu ya Pwani ya Coast General,” alisema Bw Basafar.

Mwanamke huyo, kulingana na walioshuhudia, alikuwa ameshikilia boya alipopoteza mwelekeo kwa bahati mbaya na kuanza kuzama.

“Mwanamume huyo alipoona watu wakiwa wanatapatapa mara moja aliingia baharini akijaribu kuwaokoa. Alifanikiwa lakini aliingia chini ya maji na tukampoteza, tunajaribu kumtafuta yeye au mwili wake hadi sasa,” alisema Ali Daud, mmoja wa walioshuhudia kisa hicho.

Bw Basafar alisema walipokea simu hiyo ya dhiki mwendo wa saa kumi na mbili jioni na kuwaarifu Maafisa wa Coast Guard na jeshi la wanamaji ambao walikuwa bado hawajajibu kufikia Jumamosi asubuhi.

Waziri wa Uchukuzi wa Kaunti ya Mombasa Bw Dan Manyala alibainisha kuwa wapiga mbizi wataendelea na shughuli ya utafutaji na uokoaji hadi mwanamume huyo au mwili wake upatikane.

Operesheni hiyo inaendeshwa na kikosi cha usalama na uokoaji baharini cha kaunti hiyo chenye maafisa wanaotumia maboti matatu.

Bw Basafar ametaka doria zaidi kufanywa na Maafisa wa Coast Guard akibaini visa vya kuzama majini katika fuo mbalimbali za jiji la Mombasa vimekithiri.

Watalii wa ndani na wa kimataifa wanaoingia jijini humo msimu wa sikukuu wametakiwa kuwa waangalifu.

  • Tags

You can share this post!

Wanahabari wapewa ujuzi wa masuala muhimu ya kidijitali

Diamond Platnumz amsifu Raila akisema mwanasiasa huyo ndiye...

T L