• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Mwili wa dereva wa teksi wapatikana baada ya washukiwa kuachiliwa

Mwili wa dereva wa teksi wapatikana baada ya washukiwa kuachiliwa

NA TITUS OMINDE

MAHAKAMA ya Eldoret imewaachilia washukiwa wawili kuhusiana na kutoweka kwa dereva wa teksi ambaye gari lake lilipatikana katika mtaa wa Kapsoya siku mbili zilizopita.

Lakini saa chache baada ya kuachiliwa kwa washukiwa hao wawili, mwili wa dereva wa teksi aliyetoweka ulipatikana katika shamba la majanichai eneo la Chepsonoi kando ya barabara ya Eldoret-Kapsabet katika Kaunti ya Nandi.

Akithibitisha kisa hicho Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Ainabkoi Alloys Mathoka alisema mwili wa Patrick Muiruri ulipatikana ukiwa umetupwa kwenye shamba la majanichai eneo la Chepsonoi na umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Kapsabet.

“Inasikitisha kwamba mtu ambaye teksi yake ilipatikana katika mtaa wa Kapsoya mnamo Jumapili amepatikana akiwa ameuawa katika Kaunti ya Nandi. Wapelelezi wetu wanachunguza kisa hicho ili kubaini jinsi marehemu alivyokumbana na kifo chake,” Bw Mathoka alisema.

Bw Mathoka alielezea matumaini yake kwamba ukweli utabainika hata baada ya mahakama kuwaachilia washukiwa kinyume na ombi la maafisa wa uchunguzi.

Bw Mathoka alifichua kuwa polisi watawakamata tena washukiwa hao na kuwafikisha kortini kujibu mashtaka ya wizi wa kimabavu uiliosababisha mauaji ya mwathiriwa.

“Kufuatia yaliyotokea sasa tutawakamata tena washukiwa na kuwafungulia mashtaka ya wizi wa kimabavu uliosababisha mauaji ya mwathiriwa,” alisema Bw Mathoka.

Wakizungumza katika mahakama ya Eldoret mnamo Jumatatu jioni baada ya kuachiliwa kwa washukiwa hao, viongozi wa chama cha Madereva wa Teksi mjini Eldoret walidai mahakama iliharakisha kuwaachilia washukiwa hata baada ya polisi kutuma maombi ya kuwazuilia kwa siku saba hadi uchunguzi ukamilike.

“Tunasikitika sana jinsi mahakama inavyoshughulikia suala hili. Inasikitisha kwamba polisi wanajitahidi kadiri wawezavyo kuchunguza suala hili lakini mahakama inawavunja moyo kwa kumwachilia washukiwa kabla ya kukamilika kwa uchunguzi,” alisema Luka Maina, mwenyekiti wa wahudumu wa Teksi mjini Eldoret.

Diwani wa Langas Peter Muya, ambaye aliandamana na wahudumu wa teksi nje ya mahakama ya Hakimu Mkuu wa Eldoret alionyesha kushtushwa na jinsi mahakama hiyo inavyoshughulikia kesi hiyo.

“Tunaheshimu sheria, lakini lazima mahakama zizingatie mateso ya kiakili ambayo yameathiri familia ya marehemu na madereva wa teksi katika mji huu kuhusiana na tukio hili,” alisema Bw Muya.

Alisema inashangaza kuwa washukiwa hao waliachiliwa kabla ya dereva wa teksi kujulikana aliko.

Mke wa marehemu Grace Muiruri alisema mumewe alikuwa ametoweka kwa siku tano na juhudi za kumtafuta hazikuzaa matunda kwani simu yake ilikosa kujibiwa.

Bi Muiruri sasa analilia haki.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamuziki Vivian afunguka sababu za ndoa yake na Sam West...

Presha kwa Olunga aangike daluga au afufue makali yake ya...

T L