• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Njaa yafanya wanaoishi na virusi vya HIV kususia ARVs

Njaa yafanya wanaoishi na virusi vya HIV kususia ARVs

NA SAMMY LUTTA

WAATHIRIWA wa virusi vya HIV katika Kaunti ya Turkana wamesitisha kutumia Dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs) kutokana na umaskini na njaa, hali ambayo wasimamizi wanasema kuwa pigo kubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Eric, 50, mwathiriwa wa HIV kutoka kijiji cha California, mjini Lodwar alisema ameishi na virusi hivyo kwa miaka 9 bila ya kupata chakula na kuandamwa na umaskini.

Alisema kuwa maskini na kuishi karibu na mji wa Lodwar imekuwa changamoto kupata anayemjulia hali nyumbani kwake na kumpa chakula ikilinganishwa na wale wanoishi vijijini.

“Natumia dawa za ARVs bila kula chochote na kunifanya mdhaifu. Siwezi tembea kuombaomba chakula mikahawani na kwa wapita njia,” alisema Bw Eric.

Bw Eric alisema anaelewa umuhimu wa dawa hizo kupunguza makali ya virusi, ila kutokuwa na uwezo wa kupata chakula kunaweza sababisha kulegea kupambana na viini hivyo iwapo atakosa au kuchelewa kumeza vidonge vyake.

Mwaka 2022, Idara ya Afya ya Kaunti ilikadiria jumla ya watu 19,783 wanaoishi na HIV lakini 10,708 pekee wapo kwenye tiba ya kurefusha maisha (ART).

Hata hivyo, Mratibu wa Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Magonjwa ya Mlipuko, Joseph Simiyu, alihofia kuwa kutofuata kanuni za matibabu kunaweza kusababisha dawa hizo kukosa nguvu na kushindwa kufikia kiwango cha juu cha ukandamiza virusi.

“Washikadau wanaohusika wanapaswa kufanya kazi kwa karibu ili kushughulikia makali ya njaa. Wakati uo huo, wagonjwa binafsi wanapaswa kufikiwa kupitia njia kadhaa kutoka vituo vya afya hadi kijiji ili kujua changamoto za kipekee wanazopitia,” Bw Simiyu alisema.

Akizungumza katika bustani la Moi mji wa Lodwar, Kamishna wa Kaunti Jacob Ouma alisema Wizara ya Mambo ya Ndani imejitolea katika vita dhidi ya ugonjwa huo, kwa kuhakikisha vikundi vilivyopangwa vya waathiriwa wa HIV vimeorodheshwa na kusaidiwa katika mpango usambazaji wa chakula cha msaada.

“Serikali ya Kaunti, Serikali ya Kitaifa, mashirika ya kidini na washirika wa maendeleo lazima tushirikiane ili kushinda vita dhidi ya HIV. Kupitia njia zilizopo, tunatoa chakula cha msaada kinacholenga wagonjwa masikini wasio na chakula ili waendelee kutumia ARVs bila kukatishwa tamaa,” alisema Bw Ouma.

Alitoa wito wa kuwepo na ushirikiano wa kukabiliana na unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na Ukimwi.

Afisa Mkuu wa Kaunti ya Kinga na Kukuza Afya, Peter Lomorukai aliangazia umuhimu wa kuwashirikisha vijana wa kiume katika tohara ya kimatibabu, hatua inayochangia kupungua kwa maambukizi hayo kwa asilimia 60.

Alisema licha ya kupungua, kwa sasa kuna maambukizi mapya ya HIV kutoka 600 2021 hadi 542 mwaka 2022, vijana wa miaka 10-24 na vijana wakichangia kwa asilimia 62.

Aliwataka vijana kuchukua hatua za kujikinga ili kupunguza hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa kama vile HIV na mimba za mapema.

“Wengi wa vijana wetu wameambukizwa na viashirio vya hali ya juu vinavyohusisha mwenendo na utumiaji mdogo wa kondomu. Vijana wa kiume wanapaswa kukumbatia tohara,” alisema Bw Lomorukai.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa Juja waisuta serikali kwa utepetevu fisi...

Itumbi akanusha madai kwamba Rais Ruto kaandamana na ujumbe...

T L