• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Wakazi wa Juja waisuta serikali kwa utepetevu fisi wakiendelea kuua wanakijiji

Wakazi wa Juja waisuta serikali kwa utepetevu fisi wakiendelea kuua wanakijiji

NA MWANGI MUIRURI

WAKAZI wa Juja wameingiwa na hofu baada ya fisi kumla mwanamke wa umri wa miaka 46, wiki moja baada ya kisa cha mtoto wa umri wa miaka 10 kuuawa na wanyama hao hatari.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Utawala (NGAO), mwanamke huyo alikuwa akielekea kutafuta riziki ya kuchuna kahawa katika shamba moja ambapo alikuwa akitembea kwa miguu mwendo wa saa kumi na moja alfajiri Jumamosi alipovamiwa na fisi hao.

“Wahudumu wa bodaboda walijaribu kumwokoa, lakini walikuwa tayari wamechelewa hivyo akaaga dunia kutokana majeraha ya kubururwa na kuumwa huku akiwa ameraruliwa vibaya na baadhi ya viungo vyake kuvunjwa,” ripoti hiyo yasema.

Naibu Kamishna wa Juja Bw Charles Muriithi aliambia Taifa Leo kwamba hali ya fisi hao kusambaza taharuki miongoni mwa jamii imevuka mipaka.

“Tumekuwa kukitoa tetesi zetu kwa Idara ya Huduma kwa Wanyamapori (KWS) iwajibikie hawa wanyama wao lakini hakuna afueni ambayo tumepata. Jinamizi hili limetuandama kwa miaka mingi na wananchi sasa wanalia vikali kuhusu uvamizi huu wa fisi,” akasema Bw Muriithi.

Wiki jana kijana wa Gredi ya Tano aliuawa na fisi. Alikuwa mtoto wa Peter Ngugi ambaye ni diwani wa awali wa wadi ya Witeithie.

Fisi hao wamerekodiwa kuwa na makao yao katika vijiji vya Kigwi, Muhindi, Murigu, na Benver.

“Ni ukweli kwamba hadi sasa tumepoteza makumi ya maisha katika eneo hilo kwa sababu ya fisi. Wakati wa kusaka afueni ya kudumu ni sasa,” akasema Bw Muriithi.

Alisema kwamba makao ya fisi hao ni shamba la mtu binafsi lakini ameliachilia kuwa kichaka na serikali itatafuta mbinu ya kuhakikisha fisi hao wametimuliwa.

Ingawa hivyo, baadhi ya wenyeji wameikosoa serikali wakidai utepetevu wake unaonyesha imekuwa shabiki huku wenyeji wakigeuzwa mlo wa fisi.

  • Tags

You can share this post!

Carrol Sonie, Mulamwah waambiwa watoto si wa kuingizwa kwa...

Njaa yafanya wanaoishi na virusi vya HIV kususia ARVs

T L