• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Itumbi akanusha madai kwamba Rais Ruto kaandamana na ujumbe wa maafisa 367 katika kongamano kuu la COP28 licha ya kuahidi kukata matumizi ya serikali

Itumbi akanusha madai kwamba Rais Ruto kaandamana na ujumbe wa maafisa 367 katika kongamano kuu la COP28 licha ya kuahidi kukata matumizi ya serikali

NA CHARLES WASONGA

BLOGA anayeegemea upande wa serikali ya Kenya Kwanza Dennis Itumbi amelalamika akisema madai kwamba Rais William Ruto alisafiri na ujumbe wa maafisa 367 kwa Kongamano Kuu la 28 la Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, si ya kweli.

“Rais Ruto anatekeleza mpango wa kubana matumizi ya serikali. Aliletewa listi ya watu 189 wa kuandamana naye kwa Kongamano Kuu la COP28 jijini Dubai. Alisisitiza majina yapunguzwe. Akarudishiwa listi ya 144 ambapo alisisitiza majina zaidi yadondoshwe hadi chini ya watu 60. Hatimaye ni maafisa 51 pekee waliosafiri,” akachapisha Bw Itumbi.

Bloga huyo alisema hayo baada ya madai kuibuka kwamba Rais Ruto aliandamana na ujumbe mkubwa wa maafisa wake katika mkutano wa kimataifa, baadhi yao ikiwa hawahusiki moja kwa moja na dhima ya mkutano wenyewe.

Madai hayo yaliwakera Wakenya ambao wanafinywa na ugumu wa maisha.

Duru zilikuwa zimeambia Taifa Jumapili kwamba Dkt Ruto ambaye aliondoka nchini Alhamisi kuhudhuria Kongamano Kuu la 28 la Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi jijini Dubai, katika Umoja wa Milki ya Kiarabu (UAE), aliandamana na ujumbe wa maafisa 367.

Ujumbe ulioko jijini Dubai unajumuisha Mama wa Taifa Rachel Ruto, na watoto wao Stephanie Ruto, Charlene Ruto na June Ruto.

Wengine ni mke wa Naibu Rais  Rigathi Gachagua, Dorcas Gachagua na mawaziri watano ambao ni Profesa Njuguna Ndungu (Fedha), Rebecca Miano (Biashara), Aisha Jumwa (Jinsia), Davis Chirchir (Kawi), Susan Nakhumicha (Afya), na Soipan Tuya (Mazingira).

Maafisa wengine wanaoandamana na Rais Ruto ni pamoja na Katibu wa Wizara Festus Ng’eno (Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi), Mary Muthoni (Afya), Koriri Sang’oei (Masuala ya Kigeni), Salome Wairimu (Idara ya Magereza), na Chris Kiptoo (Fedha).

Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli pia wako kwenye ujumbe wa wawakilishi wa Kenya katika kongamano hilo kuu la COP28.

Jumla ya magavana 17 pia wanahudhuria kongamano hilo la wakiongozwa na mwenyekiti wa baraza lao (CoG) Anne Waiguru (Kirinyaga).

Wengine ni Ahmed Abdullahi (Wajir), Andrew Mwadime (Taita Taveta), Benjamin Cheboi (Baringo), Kahiga Mutai (Nyeri), Gladys Wanga (Homa Bay), Susan Kihika (Nakuru), Cicily Mbarire (Embu), Erik Mutai (Kericho), na Gavana wa Garissa.

Pia wapo, magavana Wavinya Ndeti (Machakos), Wilber Ottichilo (Vihiga), Paul Otuoma (Busia), Stephen Sang (Nandi), Issa Timamy (Lamu), Patrick Ole Ntutu (Narok) na Gideon Mung’aro.

Maseneta wanaoandamana na Rais Ruto Dubai ni Joseph Githuku (Lamu), Wakoli David (Bungoma) na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’ .

Orodha hii ya ujumbe wa Kenya ilitolewa na Afisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.

Rais Ruto anaandamana na ujumbe mkubwa katika ziara ya ng’ambo mwezi mmoja baada ya yeye kutangaza kuwa serikali itapunguza bajeti ya usafiri kwa kima cha Sh11 bilioni.

Akiongea mjini Voi, kaunti ya Taita Taveta mnamo Oktoba 26, 2023, Rais Ruto alisema kuwa serikali yake inalenga kupunguza bajeti ya usafiri katika matawi yake yote matatu kwa kima cha asilimia 50 ili kuelekeza fedha zaidi kwa shughuli zenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

“Tumeamua kuwa ziara zitakazofadhiliwa kwa fedha za umma ni zile zinazolenga manufaa ya kifedha, yanavutia wawekezaji na manufaa mengine kwa raia wa Kenya,” Rais Ruto akakariri.

Amri ya kiongozi wa taifa ilijiri baada ya malalamishi kuibuliwa kuhusu ziara nyingi ambazo amefanya ng’ambo tangu alipoingia afisini mnamo Septemba 13, 2022.

Ziara hii ya Dubai ni ya 41 kwa Rais Ruto kufanya nje ya nchi tangu wakati huo.

  • Tags

You can share this post!

Njaa yafanya wanaoishi na virusi vya HIV kususia ARVs

Watu wanne wafariki kwa kuangukiwa na mbao za ghorofa...

T L