• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Pigo kwa Ruto mpango kupeleka askari 1, 000 Haiti ukizimwa na korti

Pigo kwa Ruto mpango kupeleka askari 1, 000 Haiti ukizimwa na korti

NA RICHARD MUNGUTI

SERIKALI ya Rais William Ruto imepata pigo baada ya Mahakama Kuu kusimamisha mpango wa kuwapeleka maafisa 1,000 wa polisi Haiti kudumisha amani.

Jaji Enock Chacha Mwita alitoa agizo hilo kufuatia kesi iliiyowasilishwa na Chama cha Thirdway Alliance Kenya (TAK) na Bw Miruri Waweru.

Akizima kupelekwa kwa maafisa hao nchini Haiti ambapo magaidi wamekuwa wakitesa umma, Jaji Mwita alisema kesi iliyofikishwa mbele yake na TAK na Bw Miruri ina mashiko ya kisheria.

Aidha, Jaji Mwita alifahamishwa kwamba maafisa hawa wa polisi wa Kenya hawana uzoefu na ujuzi wa kutosha kupambana na magenge yanayosumbua nchi hiyo.

“Maafisa hawa wa polisi wanaopelekwa Haiti wanakodolewa macho na changamoto nyingi, kuu ikiwa ni pamoja na kuhatarisha maisha yao,” Jaji Mwita alielezwa na TAK.

Jaji huyo aliombwa kuokoa polisi alioelezwa hawana ujuzi wa kutosha kumenyana na mibabe wa majambazi wanaodhibiti Haiti.

Mahakama imefahamishwa uamuzi wa kuwapeleka polisi nchini humo uliafikiwa baada ya kupitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Kimataifa, ndio UN Security Council.

Katika kesi hiyo, TAK imewashtaki Waziri wa Usalama Prof Kithure Kindiki, Maspika wa Mabunge ya Kitaifa na Seneti.

Jaji Mwita aliratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamuru TAK iwakabidhi washtakiwa nakala za kesi hiyo katika muda wa siku tatu na kuamuru kesi isikizwe Oktoba 24, 2023.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kindiki hata hivyo ametangaza kwamba mabunge yote mawili; La Kitaifa na Seneti, yataidhinisha au kukataa maafisa wa polisi wa Kenya kutumwa Haiti.

Pendekezo la Rais Ruto liliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Kimataifa, mataifa mawili wanachama wa baraza hilo (China na Urusi) yakikataa kupiga kura kuunga au kukataa.

Rais wa Amerika, Joe Biden pia alisifu taifa la Kenya kwa hatua hiyo aliyoitaja kuwa ya kijasiri.

Haiti imekuwa ikishuhudia ghasia na machafuko tangu 2021, baada ya Rais wa nchi hiyo Jovenel Moïse kuuawa.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Ukatili: Mama akiuawa mbele ya wanawe Nakuru

Raia wa Tunisia aliyepatikana na pesa feki atakiwa kortini...

T L