• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:21 PM
Ukatili: Mama akiuawa mbele ya wanawe Nakuru

Ukatili: Mama akiuawa mbele ya wanawe Nakuru

NA JOHN NJOROGE

POLISI eneo la Kuresoi Kaskazini, Nakuru wameanzisha uchunguzi kufuatia kisa ambapo mwanamke aliuawa kinyama mbele ya watoto wake Jumatatu Oktoba 9, 2023.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Kuresoi, Juddah Gathenge alisema hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo ya mwanamke mwenye umri wa miaka 30.

Ukatili huo unasemekana kuchochewa na masuala ya mahusiano ya kimapenzi.

Wakazi waliofika nyumbani kwa mama huyo, waliambia Taifa Leo Dijitali kushangazwa na tukio hilo la kinyama.

Bi Yvinne Cheruiyot, jirani, alisema alipata habari hizo kupitia msichana wake wa miaka tisa ambaye alikuwa amemtuma kuchukua brashi ya kufua nyumbani kwa marehemu.

“Mtoto wangu alirejea mbio akisema kuwa shangazi yake bado alikuwa kitandani, haongei na alikuwa na damu usoni,” alisema Bi Cheruiyot.

Kwa mujibu wa masimulizi, alipoenda kwake alishangaa kuona mama huyo akitokwa na damu, akiwa kitandani na alipokagua hali akaona huenda ikawa alikuwa ameaga.

Akizungumza kwa mshtuko, Bi Cheruiyot alisema alichukua hatua ya kupiga nduru kuitisha msaada.

Kulingana na jirani huyo, marehemu akiwa hai alikuwa akizozana mara kwa mara na mumewe.

“Wameishi kwa kuzozana. Tunashukuru Mungu wanawe wangali salama, hawakushambuliwa,” alielezea.

Duru zinaarifu kwamba siku moja kabla ya tukio, wakaazi walimsikia jamaa anayeshukiwa kusababisha maafa akiulizia aliko mke wake.

Mjomba wa mwendazake, David Sigei alisema mama huyo alipewa kipande cha ardhi na babake ambaye alimjengea nyumba baada ya kuondokea ndoa yake ya kwanza.

“Tunaomba askari wafanye hima kuchukulia hatua kali kisheria mhusika wa mauaji hayo ya kinyama, ambaye ametoroka,” Bw Sigei akaambia Taifa Leo Dijitali.

Bw Joel Marusoi, mwanachama wa Mpango wa Nyumba Kumi alisema marehemu alipata majeraha kichwani na uso ulijaa damu.

“Inaonekana aliuawa kwa kugongwa au kudungwa kwa kifaa chenye ncha kali. Hata hivyo, tunaomba wenyeji wawe na utulivu na subira askari wakiendeleza uchunguzi,” Marusoi akasema.

Bi Juddah Gathenge, Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Kuresoi, alisema mwili wa marehemu ulipelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali Ndogo ya Molo, ukisubiri kufanyiwa upasuaji ili kubaini kiini cha maafa.

 

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Ken Lusaka alalamikia siasa za kaunti kutishia utendakazi...

Pigo kwa Ruto mpango kupeleka askari 1, 000 Haiti ukizimwa...

T L