• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
Polisi wawili wauawa na Al-Shabaab katika Kaunti ya Mandera

Polisi wawili wauawa na Al-Shabaab katika Kaunti ya Mandera

NA MANASE OTSIALO

MAAFISA wawili wa polisi wameaga dunia huku wengine watano wakijeruhiwa kwenye shambulio la kigaidi katika Kaunti ya Mandera mnamo Ijumaa.

Shambulio hilo limetokea kwenye barabara ya Elele-Takaba katika kaunti ndogo ya Mandera Kusini saa nne asubuhi.

Chanzo kutoka kwa maafisa wa usalama kimesema msafara wa maafisa wa kitengo kilicho Elele wameshambuliwa na wanaoshukiwa kuwa ni wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab.

Kikosi hicho kilichokuwa kikipiga doria kimerushiwa gruneti na maafisa wawili waliokuwa kwenye gari wakaangamia. Maafisa watano wamenusurika kifo lakini wakapata majeraha.

Akithibitisha kutokea kwa shambulio hilo, Kamishna wa Kaunti ya Mandera Amos Mariba vikosi mseto vya maafisa vinawinda magaidi hao.

“Shambulio limetekelezwa saa nne asubuhi ambapo limewalenga maafisa waliokuwa wakishika doria. Ni jambo la kusikitisha kwamba maafisa wawili wameaga dunia. Tumeimarisha usalama na doria katika eneo hili,” Bw Mariba ameambia Taifa Leo kwa njia ya simu.

Aidha, amesema waliojeruhiwa wamesafirishwa hadi jijini Nairobi. Miili ya walioangamia pia imesafirishwa kwa ndege hadi Nairobi, amesema Bw Mariba.

Wiki jana afisa mmoja wa polisi wa akiba aliuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Guticha, Mandera na washukiwa wa Al-Shabaab.

Inadaiwa washambuliaji hao walimtuhumu afisa huyo kwa kufanyia serikali kazi na kuripoti mienendo yao katika eneo la Guticha.

Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki leo Ijumaa amezuru Kaunti ya Garissa ambapo ameapa kwamba serikali itatumia nguvu zote kukabili Al-Shabaab. Ameahidi bajeti ya Sh20 bilioni kupiga jeki maafisa wa usalama.

“Serikali imewatengea maafisa wa usalama Sh20 bilioni ili waweze kupata vifaa vya kisasa na kukabiliana vilivyo na magaidi na wahalifu,” amesema Profesa Kindiki.

  • Tags

You can share this post!

Wetang’ula asuta Azimio

Mahakama yaambiwa Mackenzie aliongoza ibada za kuwazika...

T L