• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 9:59 AM
Raila: Ni kinaya serikali ya Ruto kutoza vijana ada kupata vitambulisho ikidai inawainua kimaendeleo    

Raila: Ni kinaya serikali ya Ruto kutoza vijana ada kupata vitambulisho ikidai inawainua kimaendeleo    

NA WYCLIFFE NYABERI

KINARA wa chama cha ODM, Raila Odinga amekashifu vikali mipango ya serikali ya kutaka kuongeza ada za kuchukua vitambulisho vya kitaifa.

Bw Odinga, kwenye ziara yake ya Nyamira mnamo Jumatatu Novemba 27, 2023, alisema ni haki ya kila Mkenya aliyehitimu miaka 18 kupokea stakabadhi hiyo muhimu bila kulipia chochote.

Hivyo, kiongozi huyo wa upinzani alisema mipango ya kutoza Wakenya ada za vitambulisho, pamoja na tozo zingine inafaa kukataliwa.

Odinga alizuru Nyamira kuongoza shughuli ya usajili wa wanachama wapya wa chama chake cha chungwa, na alidokeza kuwa wabunge wa Azimio wanapanga kupeleka Mswada bungeni kutaka vitambulisho viwe vikipeanwa bila gharama yoyote.

“Kuna vijana wengi sana ambao wamehitimu miaka 18 na hawana vitambulisho, wanatembea kama wahalifu. Wanashikwa wakati hawana vitambulisho. Kitambulisho ni haki ya kila Mkenya maanake hii ndiyo thibitisho kuwa wewe ni Mkenya. Haitakikani tena ulipishwe pesa. Vitambulisho vinafaa vipeanwe bure na tunataka viwe bure. Wabunge wetu watapeleka huu mswada bungeni ili iwe sheria, isiwe eti Bw kindiki anatangaza anavyotaka,” Odinga alisema huku umati ukimshangilia.

Prof Kithure Kindiki ndiye Waziri wa Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali, na mapendekezo ya ada zinazotozwa kupata kitambulisho, pamoja na mengine, yalitangazwa na Wizara yake.

Kama ilivyo desturi yake, Waziri huyo Mkuu wa zamani hakuchelewa kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza, akisema imeshindwa kutimizia Wakenya ahadi ilizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2022.

“Wameshindwa kabisa kufanya jambo lolote. Wamekabwa kooni na skendo na kila kitu wanachoshika kinaoza. Hawajui cha kufanya ila kuongeza ushuru (VAT) kila mara. Mmejionea katika mtihani wa KCPE ambapo wanafunzi wanapewa alama sawa katika somo moja. Huo ni mtihani wa aina gani sasa?” Odinga aliuliza.

Akizungumzia ripoti ya Kamati ya Mazungumzo kuhusu Maridhiano (NADCO), kigogo huyo wa kisiasa nchini alisema, atatoa taarifa yake kesho, Jumatano, Novemba 29, 2023 na siku itakayofuatia, (Alhamisi Novemba 30, 2023), atakutana na wabunge wote wa Azimio kuwajuza mwelekeo watakaoufuata.

Alisihi wafuasi wake hasa vijana kujiandikisha kama wanachama wa ODM kwa wingi ili kuzua mchecheto chamani.

“Ndio sababu nataka tujitayarishe. Chama chetu kiwe na nguvu. Tunataka vijana waingie kwenye chama. Vijana ndio nguzo ya chama. Mnajua tangu tufanye usajili wa mwisho, miaka mitano imeisha. Kuna watu ambao wakati huo walikuwa miaka 13 lakini sasa wamefikisha 18,” Bw Odinga alisema.

Kwenye ziara hiyo, Odinga aliandamana na baadhi ya viongozi kutoka eneo la Gusii ambao wanaegemea upande wake.

Nao ni: Simba Arati (Gavana Kisii), Okong’o Mogeni (Seneta Nyamira) wabunge Clive Gisairo (Kitutu Masaba), Patrick Osero (Borabu), Irene Mayaka (mbunge maalum) miongoni mwa vongozi wengine.

Usajili wa wanachama wa ODM unatarajiwa kuendelea katika kaunti jirani ya Kisii leo, Jumanne.

  • Tags

You can share this post!

Wito marupurupu ya walimu yasawazishwe

Wasiwasi wafugaji Narok wakihadaiwa kwa chang’aa kama...

T L