• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Ruto afufua makato ya nyumba, mara hii akiendea watu wa vibarua

Ruto afufua makato ya nyumba, mara hii akiendea watu wa vibarua

Na DAVID MWERE

WAKENYA ambao ni wafanyabiashara au wamejiajiri sasa wamefikiwa baada ya mswada kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa ili nao pia walipe ada ya nyumba za gharama nafuu.

Wafanyakazi ambao wana ajira rasmi ndio wamekuwa wakikatwa ada hiyo tangu iasisiwe na utawala wa Rais William Ruto. Mswada wa Nyumba 2023 umewasilishwa bungeni baada ya Mahakama Kuu kusema kwamba ule uliokuwa ukitekelezwa, ulikuwa kinyume cha sheria na haukuwa ukizingatia msingi wa haki.

Ada hiyo ilianza kutekelezwa baada ya Sheria ya Fedha kukumbatiwa huku wafanyakazi ambao wana ajira wakiwajibikia makato yake kila mwezi.

Mswada wa sasa ambao unadhaminiwa na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah pia unalenga kuoana na uamuzi wa Mahakama ya Juu ambao uliharamisha ada ya nyumba.

Aidha mswada huo unapendekeza kubuniwa kwa Hazina ya Nyumba za Gharama nafuu ambapo ada za kila mwezi zitakuwa zikielekezwa na kusimamiwa na bodi maalum.

“Ada ya nyumba itakuwa asilimia 1.5 ya mshahara wa mtu ambaye ameajiriwa au mapato ambayo mtu amepokea,” ikasema mswada huo ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni.

Rais William Ruto analenga kujenga nyumba 200,000 za bei nafuu kila mwaka na ameahidi kuwa shughuli hiyo itakuwa ikibuni kati ya nafasi za ajira 600,000 na milioni moja kila mwaka.

Katika bajeti ya mwaka huu, Bunge iliamrisha Sh73 bilioni zielekezwe kwenye mradi huo ambao unalenga kuhakikisha Wakenya wote wana makao yanayostahiki na wanamiliki nyumba zao.

Kwa kulenga mapato ya wale ambao hawana ajira rasmi au si watumishi umma, serikali inalenga kuwiana na uamuzi wa Mahakama Kuu ambao ulisema kuwa ilikuwa ubaguzi kuwataka walioajiriwa pekee wachangie ada ya nyumba.

Wale ambao wamejiajiri au wana njia zao za kupata mapato watahitajika kulipa pesa zao kufikia tarahe tisa ya kila mwezi.

Mahakama pia ilisema mswada wa awali kabla uwe sheria haukuwa unazingatia katiba kutokana na umma kukosa kushirikishwa wakati wa utoaji maoni.

Mswada ambao upo bungeni kwa sasa kupitia mchakato unaohitajika kisheria utashirikisha Wakenya kualikwa watoe maoni yao.

  • Tags

You can share this post!

Afisa asimulia kisa cha kushangaza kuhusu...

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Maadili yako wapi, tunafunza nini...

T L