• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Maadili yako wapi, tunafunza nini kizazi kijacho?

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Maadili yako wapi, tunafunza nini kizazi kijacho?

Na ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Tumejaaliwa leo hii kukutana katika jukwaa hili la kukumbushana na kuelimishana kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Ama kabla ya kujitosa kwenye mada ya leo, sharuti tumpwekeshe, kumwabudu, kumcha na kumshukuru mwisho wa shukrani Mola wetu. Ni yeye pekee, Allah (SWT) Anayestahili kuabudiwa. Ni yeye pekee, Mwenye-Enzi, ndiye Muumba wa ardhi na mbingu; na vyote vilivyomo.

Baada ya kumpwekesha na kumtukuza Mola wetu mmoja, sawia tunachukua uzito wa nafasi hii kumtilia dua na kumfanyia kila aina ya maombi Mtume wetu (SAW).

Ukurasa wetu wa mawaidha tunaufungua leo hii kwa kuzidisha dua na swala maalum kwa ndugu zetu huko Gaza. Baada ya siku chache za utuvu na kuachiwa huru kwa mateka, sasa hivi tena kunashuhudiwa mashambulio na mauaji kutoka kwa Israel dhidi ya Wapalestina. Hali katika ukanda wa Gaza ni tete mno!

Vivyo hivyo, makabiliano na uvamizi wa silaha kali kali vingali vinashuhudiwa katika nchi ya Ukraine kutoka kwa Urusi. Vita hivi vimeathiri mno uchumi wa dunia; kusababisha vifo na madhara chungu nzima kwa waja; sikwambii kuzidisha chuki miongoni mwa wanaulimwengu!

Ya Rabi!

Ndio maana nchi zinazidisha kuvumba silaha kali zenye kemikali na kujihami mno! Kisa na maana? Huwezi ukajua jirani yako anakupangia nini. Mauaji haya, hasa kwa watoto, wanawake, wazee – nchi zinavunja kaida na kanuni za vita – yanaendelea huku wengine wetu wakisema tu: LANGU JICHO! Maskini binadamu. Kuuana wenyewe kwa wenyewe.

Vipi huko Sudan? Hali ni piga ua.

Hii inaonesha ni kwa namna gani utu umetutoka sisi waja. Hakuna hata chembe cha maadili. Nchini mwetu majuzi kumetangazwa matokeo ya mtihani wa darasa la nane, KCPE, huu ukiwa mtihani wa mwisho wa mfumo wa elimu wa 8-4-4, kwa darasa la nane.

Huku wengine wakisherehekea matokeo yao, baadhi nao wanalia. Kwa nini?

Wnafunzi walipata alama za masomo ambayo hawakufanya kamwe. Kulikoni? Hii inatoa picha gani kwa mchakato mzima wa uteuzi wa shule za upili? Hali ni mchafukoge. Hakuna uaminifu. Hapana uwajibikaji.

Hakuna maadili. Kinachoendelea na waziri husika na katibu wake kuhojiwa hapa na pale. Wazazi na wanafunzi waliojeruhiwa wakisaga meno na kushtaki wahusika.

Kama hilo halitoshi, baadhi ya viongozi, wanasiasa, wanalimana na kurushiana matusi na kupasuliana magari hadharini. Yaani hali ni kila mtu na nguvuze. Uongozi unadorora kila kukicha. Kila mmoja anapapia maisha na kuikimbilia roho.

Maadili yako wepi katika jamii yetu? Tunawafunza nini watoto, vijana na kizazi kijacho? Mitandao na vyombo vya habari vimejaa uhuni, uchi na utupu?

Maadili ya wapi? Ya Allah (SWT) tunusuru. Tunaangamia!

Ijumaa Mubarak

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Ruto afufua makato ya nyumba, mara hii akiendea watu wa...

Bobi Wine ashambuliwa kwa madai yake kuhusu sheria ya...

T L