• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Ruto anavyolenga kupokonya Raila Baraza la Waluo

Ruto anavyolenga kupokonya Raila Baraza la Waluo

Na RUSHDIE OUDIA na CHARLES WASONGA

KUCHELEWESHWA kwa uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo kuchukua nafasi ya Mzee Willis Otondi kumeibua wasiwasi huku uvumi ukienea kuwa Rais William Ruto anapania kuingilia shughuli hiyo.

Duru zinasema kuwa wandani wa Dkt Ruto kutoka Luo Nyanza wanaendesha kampeni za kumpigia debe mzee wanayempendelea kuchukua wadhifa huo, maarufu kama “Ker”.

Viongozi hao wanaoegemea mrengo wa Kenya Kwanza wanataraji kuwa Mzee huyo akifaulu kutwaa kiti hicho chenye hadhi, watafaulu kunadi ajenda za Rais Ruto kwa urahisi katika eneo zima la Luo Nyanza.

Katika siku za hivi karibuni, Waziri wa Teknolojia ya Habari na Utangazaji (ICT) Eliud Owalo, Katibu katika Wizara ya Usalama Raymond Omollo, Waziri Msaidizi katika Wizara ya Biashara Evans Kidero mingoni mwa wandani wengine wa Rais Ruto wamekuwa wakikutana na Mzee Nyandiko Ongadi ambaye wanamtambua kama “Ker” halali.

Wadadisi wanasema kuwa kucheleweshwa kwa uchaguzi wa “Ker” mpya kunawafaidi washirika hawa wa Rais Ruto ambaye wanampigia debe Mzee Ongadi ashinde kiti hicho.Lakini wakati wa “utawala” wa marehemu Otondi, Mzee Ongadi alichukuliwa kama kiongozi wa kundi la wazee waasi wa uongozi wa Mzee Otondi aliyeungwa mkono na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Mzee Otondi alifariki Februari 17, 2023 akiwa na umri wa miaka 92 na kuzikwa nyumbani kwake eneo la Ahero, eneobunge la Nyando, Kaunti ya Kisumu.Mzee Ongadi anatoka eneobunge la Rangwe kaunti ya Homa Bay.

Wawaniaji

Wengine ambao majina yao yametajwa kuwa walioko kwenye kinyang’anyiro hicho ni pamoja na; Mzee Odungi Randa, mwenye umri wa miaka 82, ambaye ni aliyekuwa msaidizi wa babake Raila, Jaramogi Oginga Odinga, Mzee Odera Osawa (76) ambaye ni Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee wa Waluo na Mzee Owino Nyadi ambaye ni mkurugenzi Mkuu wa baraza hilo.

Ili mtu achaguliwe kuwa “Ker” wa baraza hilo, sharti awe na umri wa angalau miaka 60 na asijihusishe na siasa moja kwa moja.

Miongoni mwa majukumu ya Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo ni kutoa ushauri na mwelekeo kuhusu masuala yenye umuhimu kwa jamii hiyo haswa katika nyanja za kitamaduni, kiuchumi na hata kisiasa.Lakini shughuli za baraza hilo huvutia wanasiasa haswa wale wanaowania viti vya kitaifa kwa sababu uungwaji mkono kutoka baraza hilo huwaongezea ushawishi wa kisiasa katika jamii ya Waluo na hata jamii nyinginezo.

“Hii ndio maana kiongozi wa ODM Raila Odinga kila mara hutaka kuwa na usemi katika uchaguzi wa Ker kwa manufaa yake ya kisiasa,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dkt David Okello.

“Nadhani hii ndiyo maana Rais Ruto na wandani wake pia wanataka kushawishi uchaguzi wa Ker mpya atakayechukua nafasi ya marehemu Otondi ili waweze kumtumia kuyeyusha ushawishi wa Raila kisiasa katika ngome yake ya Luo Nyanza,” akaongeza Dkt Okello ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

 

  • Tags

You can share this post!

Raia wa kigeni ‘anayeuza’ watu afurushwa

Kongamano la Kitaifa la Jubilee

T L