• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Serikali kuharibu pasipoti 10,000 za waliozembea kuzichukua

Serikali kuharibu pasipoti 10,000 za waliozembea kuzichukua

NA TITUS OMINDE

ZAIDI ya pasipoti 10,000 ambazo bado hazijachukuliwa kutoka kwa ofisi ya Idara ya Uhamiaji mjini Eldoret huenda zikaharibiwa katika muda wa wiki tatu zijazo ikiwa waliotuma maombi ya kuzipokea hawatakuwa wamezichukua.

Wiki mbili zilizopita, Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki alipokuwa akitoa agizo la utoaji wa hati za kusafiria wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Matokeo ya Haraka (RRI), alionya kuwa pasipoti zinazozalishwa lazima zichukuliwe ndani ya siku 30 la sivyo ziharibiwe.

“Wanaotuma maombi ya kupokea pasipoti lazima wachukue pasipoti zao. Wale ambao hawatazichukua kama ilivyopangwa baada ya notisi kuisha tutachukulia kwamba ni hati ambazo hazina wenyewe na tutazitupa,” alisema Prof Kindiki.

Waziri huyo alionya kwamba wenye pasipoti hizo watahitajika kutuma maombi upya baada ya kulipa faini ambayo haijatajwa.

Kwa sasa ofisi ya eneo la Eldoret ambayo ni ya pili kwa idadi kubwa ya pasipoti ambazo hazijachukuliwa baada ya Nairobi, ina zaidi ya pasipoti 10,000 zinazosubiri kuchukuliwa na wenyewe.

“Tumekuwa tukifanya kazi usiku na mchana baada ya Waziri wetu kuzindua RRI, kama ofisi ya eneo hadi sasa tuna zaidi ya pasipoti 10,000 ambazo bado hazijachukuliwa,” alisema Maurice Anyanda, naibu mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji anayesimamia North Rift/Western.

Bw Anyanda alisema maafisa wake wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana ili kuharakisha utoaji wa stakabadhi hizo kama njia moja ya kutekeleza agizo kutoka kwa waziri Kindiki.

Akiwahutubia waliokuwa wametuma maombi ya kupokea pasipoti kupitia afisi ya Eldoret Bw Anyanda aliwaambia waliotuma maombi kutembelea afisi hiyo na kuchukua pasi hizo ili wazitumie kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alisema kuwa ofisi ya Eldoret inahudumia eneo kubwa kwa hivyo hiyo inaweza kuwa sababu ya uwepo wa idadi kubwa ya pasipoti ambazo hazijachukuliwa.

“Kwa sasa tuna idadi kubwa ya pasipoti ambazo wenyewe hawajazichukua. Maafisa wangu wanafanya kazi kwa zamu ili kupunguza mrundikano huo na itakuwa jambo la kutia moyo na busara zaidi kwa waliotuma maombi kuja kuchukua pasipoti zao baada ya kutuma maombi,” akasema Bw Anyanda.

Wiki tatu zilizopita, wizara hiyo ilitangaza kwamba kuna zaidi ya pasipoti 87,000 ambazo bado hazijachukuliwa kote nchini.

Waziri alisema pasipoti 87,574 zilikuwa zimetolewa kufikia mwezi Agosti na zilikuwa tayari kuchukuliwa kutoka Nyayo House.

Kulingana na takwimu za idara hiyo Nairobi inaongoza kwa zaidi ya pasipoti 40,000 ambazo hazijachukulia.

  • Tags

You can share this post!

Kinyesi cha binadamu chatumika kuzuia MCAs kumbandua gavana...

Serikali yachunguza ‘adui wa ndani’ katika mashambulizi...

T L