• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Serikali kukwamua vyuo vikuu kwa ufadhili wa Sh90 bilioni

Serikali kukwamua vyuo vikuu kwa ufadhili wa Sh90 bilioni

NA WINNIE ATIENO

SERIKALI imetenga Sh90 bilioni kwa vyuo vikuu 35 vya umma, ili kupiga jeki sekta ya elimu ya juu nchini ambavyo vilikuwa katika hatari ya kuangamia kutokana na deni na ukosefu wa ufadhili.

Vyuo hivyo vinadaiwa Sh77 bilioni.

“Wale ambao watahusika na ufisadi watachukuliwa hatua kali za kisheria. Serikali haitamsaidia yeyote ambaye atapatikana na kashfa ya ufisadi. Lazima muwe na maadili mema,” alisema Waziri wa Elimu Bw Ezekiel Machogu.

Kwa zaidi ya miaka minane, vyuo vya umma vimekuwa na changamoto za kifedha na ukosefu wa wanafunzi.
Wakuu wa vyuo vikuu wamekuwa wakiilaumu serikali kwa masaibu ambayo wamekuwa wakikumbana nayo baada ya kunyimwa ufadhili.

Hata hivyo, Bw Machogu ambaye aliongea kwenye mkutano na Wakuu wapya wa Vyuo Vikuu katika hoteli ya Sarova Whitesands Mombasa, aliwaonya dhidi ya ufujaji wa fedha za umma na ufisadi.

“Kwa miaka mingi sasa, vyuo vikuu vimekuwa vikikumbwa na changamoto nyingi hasa za uongozi na fedha ambazo zinahitaji suluhu ya dharura kutoka kwenu. Vyuo vikuu vinadaiwa Sh77 bilioni kutokana na deni la Sh60 bilioni katika kipindi cha Mwaka jana wa fedha,” alisema Waziri huyo.

Alisema deni hilo limetokana na utepetevu wa baadhi ya wakuu wa vyuo vikuu.

“Kumekuwa na madai kwamba baadhi ya wakuu wa vyuo wanaeneza uovu vyuoni hasa ukabila na uajiri wa wafanyakazi kupita kiasi badala ya wakufunzi. Hawa ni wafanyakazi ambao hawahitajiki vyuoni lakini bado wanaajiriwa,” alisema.

Bw Machogu alisema wakuu hao wamekuwa wakiajiri wafanyikazi ambao wanachukua fedha nyingi za vyuo vikuu na kuchangia taasisi hizo kukumbwa na changamoto za kifedha.

Zaidi ya hilo, Machogu alisema vyuo hivyo vimekuwa havitilii maanani masuala ya masomo, utafiti na ubunifu.

Alisema ukosefu wa uongozi bora katika vyuo hivyo umechangia taasisi hizo za elimu kushindwa kushindana na vingine vya kimataifa.

“Hatuwezi kuendelea hivi tena, lazima tubadili mkondo ili tuokoe taasisi zetu za elimu. Inasikitisha kuwa vyuo vyetu vinaendelea kushika mkia katika ngazi za kimataifa,” alisikitika.

Alitaja vyuo vikuu tajika vikiwemo Harvard, Stanford, Oxford, Cambridge, MIT, University College London na Imperial College London ambavyo Kenya inafaa kushindana navyo.

“Serikali imewekeza katika sekta ya elimu na tunawasihi mhakikishe elimu katika vyuo vikuu inaboreshwa. Mwaka huu serikali imetenga Sh90 bilioni kwa elimu ya vyuo vikuu vya umma, hizi ni fedha ambazo zikitumiwa vizuri zitapiga jeki elimu,” alisema.

Aliwataka kuwa makini ili wasihadaiwe na wafanyikazi watumie fedha vibaya.

“Muwe na elimu ya maswala ya kifedha la sivyo mtahadaiwa na nyinyi ndio mtakaoingia kwenye shimo na kuchunguzwa kwa ufisadi hatimaye kuwekwa korokoroni,” alisema Bw Machogu.

Alisema serikali imetenga Sh749 milini katika Mwaka huu wa kifedha wa 2023/2024 katika utafiti, sayansi, ubunifu na uvumbuzi.

Waziri Machogu alisema katika Mwaka huu wa Elimu 2023/2024 wanafunzi 131,373 wataingia vyuo vikuu.

“Idadi ambayo itaongezeka kutokana na mageuzi ambayo tumetekeleza katika mfumo wa elimu nchini ili kuongeza idadi ya wtaoto wetu wanaojiunga na vyuo vikuu,” alisema.

Aliwataka wahakikishe vyuo vikuu vinatoa wanafunzi waliohitimu na shahada ya uzamifu (PhD).

Alisema kwa mwaka serikali inalenga kutoa wanafunzi 1,000 walio na PhDs.

  • Tags

You can share this post!

Kwayamasta nusura aharibu ndoa yake ‘mpango’...

CDF Francis Ogolla amuomba Rais Ruto msamaha kwa kusahau...

T L