• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Serikali kupendekeza sheria ya kudhibiti soko la hewa ukaa nchini Kenya

Serikali kupendekeza sheria ya kudhibiti soko la hewa ukaa nchini Kenya

NA JACOB WALTER

RAIS William Ruto amebainisha mipango ya serikali kupitisha sheria bungeni itakayothibiti soko la hewa ukaa (Carbon credit) nchini Kenya na kukabilian na visa vya ulaghai katika biashara hiyo ambayo imeanza kunoga kote ulimwenguni.

Akiongea na Taifa Jumapili katika konagamano la Umoja wa Mataifa la mabadiliko ya tabianchi almaarufu COP28 nchini Dubai, Rais Ruto ameeleza kuwa tayari mipango kabambe iko njiani kuwasilisha hoja bungeni itakayopasishwa na kuwa sheria ya kudhibiti biashara hiyo ya hewa ukaa.

“Nina uhakika kuwa nchi ya Kenya inaongoza mataifa mengine barani Afrika katika kubuni sheria ambazo zitakuwa kuwa nguzo za kuthibiti soko la hewa ukaa,” amekariri Rais Ruto.

Serikali iko kwenye mkondo wa mwisho mwisho katika utungaji wa mswada huo utakowasilishwa bungeni katika siku karibu zijazo akiongeza kuwa tayari alitia sahihi baadhi ya mabadiliko ya vipengee vya sheria  zinazoambatana na biashara hiyo.

Aidha maswala tata ya kuthibiti bei ya bidhaa hiyo katika masoko kote nchini yameibuka huku Rais Ruto akiyakinisha kuwa Kenya inaunga mkono  mpango wa Benki ya Dunia kuthibiti soko la hewa ukaa kote ulimwenguni ili kuhakikisha usawa,haki na uwazi katika biashara hiyo ya mamilioni ya pesa.

Bw Ruto amesistiza haja ya taifa la Kenya kupanua vyanzo vingine vya mapato has katika biashara zinazoamabatana na makabiliano dhidi ya hewa ukaa.

Hata hivyo akasema kuwa sharti ziwepo sera, sheria na vigezo thabiti zitakazotawala soko hilo nchini Kenya.

Alifafanua kuwa ipo haja kuu ya sheria katika soko la hewa ukaa ili kuhakikisha kuwa bei, soko nzima na maadili katika soko hilo zimekitwa kwenye msingi thabiti.

Hata hvyo kuhusu madai kuwa kuna baadhi ya misitu kama Mau kuuziwa wawekezaji wa hewa ukaa,Rais Ruto amekanusha kuwa hakuna hata inchi  moja ua kipande cha msitu zimeuziwa wawekezaji nchini Kenya.

Ikumbukwe kuwa Machi 2023, Kenya iligonga vichwa vya habari kuhusiana na kubatilishwa kwa vyeti vya shirika kubwa nchini katika biashara hiyo ya hewa ukaa na kampuni moja ya Marekani ya kuwekeza katika biashara hiyo, kufuatia madai kuwa hawakuzingatia sheria ya kudhibiti ugavi wa mapato ya faida kutokana na biashara hiyo kwa jamii wenyeji wa ardhi.

Aidha amepongeza hatua ambazo zimepigwa na majadiliano yanayoendelea katika kongamano la COP28 huku matumaini ya mataifa maskini katika kukabaliana na mabadiliko ya nchi yakifufuliwa kutokana maagano kadhaa yaliyoidhinishwa na mataifa husika.

Hadi sasa maagano ya fidia kwa nchi zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi almaarufu ‘Loss and Damage Fund’ imepokelewa kwa shangwe na mataifa maskini huku mataifa tajiri yakitangaza Dola milioni  430 za Marekani za kuelekezwa katika mataifa wahanga.

Kongomano la COP28 limetarajiwa kufanya utathmini kuhusu hhatua zilizopigwa na mataifa ulimwengu tangu yalipoidhinishwa kwa Mapatano ya Paris mwaka wa 2015 ya mataifa yote kujitahidi kupunguza hewa chafu ya kaboni hadi nyuzijoto 1.5.

  • Tags

You can share this post!

Watu wanne wafariki kwa kuangukiwa na mbao za ghorofa...

Niliyoyachukulia ni mambo madogo tu yamenivunia heshima...

T L