• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Serikali ya UDA inasakamwa na ushindi walioniibia, Raila asema

Serikali ya UDA inasakamwa na ushindi walioniibia, Raila asema

NA SHABAN MAKOKHA

KIONGOZI wa Upinzani Raila Odinga amesema changamoto zinazoikumba serikali ya Kenya Kwanza ni kwa sababu imesakamwa na kile alichodai ni ‘kumuibia’ ushindi wake katika kura za 2022.

Bw Odinga ambaye alikuwa katika hafla ya kusajili wanachama wapya wa chama chake cha ODM Ijumaa Desemba 1, 2023 katika Kaunti ya Kakamega alishikilia kwamba yeye ndiye aliyeshinda urais dhidi ya Rais wa sasa William Ruto.

Kura ya urais ilifanyiwa uamuzi wa mwisho katika Mahakama ya Upeo ambapo ilishikilia kwamba Dkt Ruto alichaguliwa kwa kura 7.1 milioni njia halali, dhidi ya Bw Odinga 6.9 milioni, katika uamuzi ulioungwa mkono na majaji wote wa mahakama hiyo mwaka jana.

Hata hivyo, mrengo wa Azimio la Umoja ambao ndio Bw Odinga aliotumia kuwania urais akiwa na mgombea mwenza Martha Karua umeshikilia hadi leo kwamba walinyimwa ushindi (kwa mara nyingine).

Ni kauli ambayo Bw Odinga alirejelea akiwa mbele ya umati, eneo la Lurambi, Ijumaa:

“Sasa, unajua waliiba kura yetu. Si waliiba?”

Umati: “Ndio baba”

Raila: “Hata kama waliiba, imekwama kwa koo. Imekataa kuteremka. Wanatafuna lakini haiteremki. Wanafanya ..ehe..ehee..ehee”

Umati: [Kicheko]

Raila: “Inawanyonga. Si inawanyonga?”

Umati: [Kicheko] “Ndio baba”

Aliendelea na hotuba akielezea kwa nini ameanza mapema usajili wa wanachama, akifafanua kwamba huu ndio wakati mwafaka, ambao wananchi tayari wameshapoa kutokana na mishemishe za uchaguzi. Akasema kwamba ameona heri kuanza zoezi la usajili akidai kwamba kuna hatari ya mabwanyenye kumwaga pesa nyingi dakika za mwisho mwisho na kuzuga akili wapiga kura.

Katika hafla hiyo hiyo, kiongozi huyo wa Azimio ambaye amewania urais kwa mara tano bila kufanikiwa alisalia kimya pale viongozi wa ODM walipomtaka atangaze kwamba atawania tena 2027.

Viongozi wa chama hicho katika kaunti ya Kakamega walitangaza kuwa Bw Odinga ndiye chaguo lao katika kinyang’anyiro kijacho cha urais wakisema ndiye anaweza kurekebisha makosa ya utawala huu wa Rais William Ruto.

Waliisuta serikali hii kwa kuuboronga uchumi kupitia kile walichokitaja kama uporaji wa mali ya umma.

Wakiongozwa na Gavana wa Kakamega, Fernandes Barasa, viongozi hao, wakiwemo Naibu Gavana Ayub Savula na wabunge Tindi Mwale, walimtaka Bw Odinga kutoachia mtu mwingine kibarua cha kung’oa mamlakani Rais Ruto.

Walitaja ongezeko la bei za bidhaa za kimsingi kama chakula na mafuta, ubomoaji wa majengo ya kibinafsi na kukithiri kwa ufisadi kama mapungufu ya utawala wa Rais Ruto.

-Ripoti ya ziada na uhariri – FATUMA BARIKI

  • Tags

You can share this post!

Kuna wakati nilitaka kujitoa uhai sababu ya jumbe nyingi za...

Wafanyakazi ‘hewa’ waliotimuliwa na Gavana Wanga wapata...

T L