• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Umaskini walazimu vijana kutorokea ng’ambo bila stakabadhi   

Umaskini walazimu vijana kutorokea ng’ambo bila stakabadhi  

BRIAN OCHARO NA ANTHONY KITIMO

VISA vya vijana kutoka eneo la Pwani kujaribu kutorokea nchi za ng’ambo kwa kujificha ndani ya meli kama njia ya kusafiri bila stakabadhi vimeongezeka, wengi wakiwa na imani kuwa njia hiyo itawaondoa katika uchochole.

Mabw Ali Mbaraka na Hassan Ali walifika katika bandari ya Mombasa wiki mbili zilizopita wakiwa na imani kuwa wangepata mpenyo wa kubadilisha maisha yao.

Wawili hao walikuwa wakijaribu bahati yao, ili kuhamia ng’ambo na kubadilisha maisha yao na za familia zao kwa kujificha katika meli ya MV RIVER MAS.

Nyota zao za kuishi ughaibuni zilizimwa baada ya kuonekana ndani ya meli hiyo pindi tu ilipong’oa nanga katika mojawapo ya maegesho kuelekea Georgia, Amerika.

Kulingana na marafiki wao wa karibu, wawili hao wamekuwa na ndoto ya kuondoka nchini kutafuta maisha mazuri ng’ambo, ikibainika kuwa Mbarak amekamatwa kwa mara ya pili sasa akijaribu kuondoka nchini.

“Kuna marafiki wao ambao walifaulu kuhepea ng’ambo kinyume na sheria na wamekuwa wakiwasukuma wawili hao kuhama makazi yao katika kijiji cha Mtongwe, Likoni kaunti ya Mombasa. Siwezi kuzungumza mengi kwa kuwa kesi iko mahakamani,” akasema mmoja wa marafiki wao Bw Abdulrahaman Sheriff.

Walipofikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mombasa Vincent Adet, walikubali mashtaka. Waliomba serikali iwahurumie kwa kuwa walikuwa na familia zilizowategemea.

“Nina familia inayonitegemea, mimi hufanya biashara zangu kando ya Bahari Hindi,” akasema Bw Mbarak.

Bw Ali alijitetea mbele ya mahakama, akieleza kuwa alikuwa yatima na majukumu mengi.

Mahakama ilileza kuwa makosa hayo yalifanyika Agosti 24 katika bandari ya Mombasa.

Mahakama ilielezwa kuwa Mbaraka alikuwa ameshtakiwa na kosa kama hilo manmo 2022, baada ya kuabiri meli ya MV Navios Uranius, ambayo ilikuwa ikielekea Mauritius.

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya ubaharia Bw Andrew Mwangura, vijana hujaribu bahati yao nje ya nchi.

“Tuna wengi waliofaulu kuhepea mataifa ya ughaibuni na kwanza kuwepo kwa mtandao, kumewasaidia kuchapisha picha na video za maisha yao huko. Kwa sababu ya gharama ya juu ya maisha, kuna matukio mengi yanayozidi kutokea,” akasema Bw Mwangura.

Kulingana naye, “Ukosefu wa ajira kwa vijana kwa sasa ipo kwa asilimia 65, na iko miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa pakubwa na ukosefu wa ajira duniani. Huku kunachangia vijana kutorokea mataifa ya nje.”

Kwa sasa Mabw Mbaraka na Ali wanaungana na vijana wengine kutoka Pwani wanaosubiri hukumu, huku wengine wakihudumia kifungo.

Mwaka huu pekee watu watano wamekamatwa wakijaribu kutorokea mataifa ya ng’ambo.

Licha ya hayo kuna Wakenya kadhaa, walioripoti kuwasili katika mataifa hayo waliyotorokea bila kukamatwa.

Vijana hao huchagua sehemu ambazo hazikaguliwi sana katika meli hizo na wao huwa wamejihami vizuri na chakula na maji. Kuna madai kuwa wengine huwahonga wafanyakazi wa bandari ili wafumbie jicho wanapopita kwenye jeti.

 

  • Tags

You can share this post!

Mung’aro ajiita ‘Binti Kiziwi’ akisema kelele za...

Wanahabari wafurushwa Mukumu Girls bweni likiteketea

T L