• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Mung’aro ajiita ‘Binti Kiziwi’ akisema kelele za mahasimu hazimzuii kuchapa kazi Kilifi

Mung’aro ajiita ‘Binti Kiziwi’ akisema kelele za mahasimu hazimzuii kuchapa kazi Kilifi

NA MAUREEN ONGALA

GAVANA wa Kilifi Gideon Mung’aro amepuzilia mbali cheche za maneno kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama cha Orange Democratic Movement katika kaunti hiyo.

Amesema sasa ameamua kuwa ‘Binti Kiziwi’ asiyebabaishwa na maneno ya wakosoaji wake bali anayeweka zingatio kuu kwa kuwaletea maendeleo wakazi wa Kilifi.

Hii ni baada ya Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kilifi Bi Getrude Mbeyu kuanza kumkosoa gavana Mung’aro kila mara kwa umma akidai kuwa serikali yake ilikuwa inaendeleza ufisadi na kuwa amekosa kuwajiba katika kuwahudumia wakazi wa Kaunti ya Kilifi.

Pia Mbeyu ametangaza kuwa atawania kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Akizungumza wakati wa kuzindua ujenzi wa hospitali ya kisasa katika kituo cha afya cha Mtwapa, gavana Mung’aro alisema kuwa hababaishwi na cheche hizo na yeye anatilia maanani utendaji kazi wake kwa sasa.

“Nimesikia viongozi fulani wakiongea kuhusu kiongozi fulani. Hizo kelele nazijua kwa sababu naziona kila siku kwa mtandao. Lakini nataka kuwaambini mkiwaona wakipiga kelele waambieni mimi ni Binti Kiziwi. Hata wakiniambia wananipenda sisikii. Ninafanya kazi yangu ya kuwahudumia watu wa Kilifi. Wewe utapiga kelele mchana na usiku utalala,” akasema.

Tabia hiyo ya Mbeyu pia haijamfurahisha kiongozi wa walio wengi katika bunge la kaunti ya Kilifi Bw Ibrahim Matumbo ambaye alitangaza vita vikali dhidi yake.

Bw Matumbo ambaye ni diwani wa Watamu, alimkemea mwakilishi huyo wa kike na kusema kuwa anasaliti chama cha ODM.

“Inahuzunisha sana kuona gavana wetu aking’ang’ana kuhakikisha watu wa Kilifi wanapata huduma bora na huku mama wa kaunti Getrude Mbeyu anazunguka akikashifu serikali ya kaunti ambayo inaongozwa na ODM,” akasema.

Bw Matumbo alidai kuwa Mbeyu alikuwa anatumiwa na mahasidi wa gavana Mung’aro kuhujumu serikali yake kwani hana misuli ya kupambana na gavana.

“Nikiwa kiongozi wa walio wengi bungeni nimepiga marufuku Mbeyu kuzungumza katika mikutano yote ya umma itakayoandaliwa na wajumbe wa ODM waliochaguliwa na kuteuliwa hata kama ni kwa matanga au harusini,” akasema.

Aliapa kuhakisha kuwa Mbeyu anatimuliwa chamani.

“Baada ya kumalizana na Mbeyu, tutapambana na wale wanaomtuma,” akasema.

Mwenyekiti wa chama cha ODM kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire amewataka viongozi hao kudumisha nidhamu na kufanya kazi pamoja.

Bw Mwambire ambaye ni spika wa bunge la kaunti ya Kilifi alisema ni mapema sana kwa viongozi hao kuanza kutofautiana akisema kuwa hawakuwa na sababu yoyote ila ni kwa ubinafsi wao.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi Ruiru watumia mbinu za kizamani za upishi bei ya...

Umaskini walazimu vijana kutorokea ng’ambo bila...

T L