• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
UoN na mwanakandarasi wazozania malipo ya ujenzi wa mabweni yaliyoachwa mwaka 1990

UoN na mwanakandarasi wazozania malipo ya ujenzi wa mabweni yaliyoachwa mwaka 1990

NA RICHARD MUNGUTI

CHUO Kikuu cha Nairobi (UoN) kimepinga vikali kesi ambapo mwanakandarasi aliyepewa kazi ya kujenga mabweni katika Bewa la Kabete mwaka 1990 anataka alipwe Sh137 milioni kwa ujenzi wa mabweni uliosimama.

Ujenzi wa mabweni hayo ulikwama Juni 1990 mashirika ya kigeni yalipofunga mikoba kuipa Kenya misaada.

Mwanakandarasi huyo ameshtaki UoN akiomba alipwe kitita cha Sh137 milioni.

Lakini UoN kupitia kwa wakili Patrick Lutta imemweleza Jaji Profesa Nixon Sifuna wa Mahakama Kuu ya Milimani jijini Nairobi kwamba kampuni ya NK Brothers Limited ililipwa na Serikali mnamo Machi 2, 2000, na “haistahili kulipwa hata senti moja.”

“N K Brothers hawastahili kulipwa hata senti moja kwa vile walilipwa na Wizara ya Fedha yapata miaka 23 iliyopita,” akafichua msanifu majengo wa UoN Jerret Odwallo.

Jaji huyo alielezwa kwamba NK Brothers walilipwa Sh27 milioni na endapo “malipo mengine yatatolewa basi huo utakuwa ni ufisadi.”

Jaji Sifuna alielezwa Wizara ya Fedha iliandika barua ikisema “NK Brothers walipokea malipo na hawafai kudai malipo mengine.”

Katika ushahidi uliowasilishwa na Bw Odwallo, Mahakama ilielezwa kuwa NK Brothers walilipwa kwa hundi nambari 001939 ya benki ya National Bank. Hundi hiyo ilikuwa ya Sh27,965,254.60.

Malipo hayo yalifuatia muafaka uliotiwa saini kati ya NK Brothers na Serikali kwamba ipewe bima za biashara za thamani sawa na pesa ilizokuwa inakidai chuo hicho kikuu.

NK Brothers walipewa bima hizo za biashara mnamo Oktoba 19, 1999. Kufuatia makubaliano hayo, mahakama ikaelezwa sasa haina deni inalodai UoN.

Mahakama ilielezwa ujenzi wa mabweni hayo ulikwamishwa na mashirika ya kigeni kukoma kuifadhili serikali mwaka 1990 wakati wa utawala wa hayati Daniel Toroitich arap Moi.

  • Tags

You can share this post!

Serikali sasa yaweka ada ya kupata kitambulisho kuwa Sh300...

Murkomen adai mapaa yanavujisha maji JKIA kwa sababu...

T L