• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Wakulima Mlima Kenya wamtaka Gachagua awatimizie ahadi alizotoa ili wakabiliane na upinzani

Wakulima Mlima Kenya wamtaka Gachagua awatimizie ahadi alizotoa ili wakabiliane na upinzani

Na MWANGI MUIRURI 

MUUNGANO wa wakulima kutoka eneo la kati umemtaka Naibu wa Rais Rigathi Gachagua aharakishe mabadiliko kuongeza mapato ili iwe raha kushabikia serikali ya Rais William Ruto dhidi ya maandamano ya upinzani.

“Sisi tunaambiwa kwamba serikali hii ni yetu eti kwa sababu Gachagua na Agikuyu wengine wamepewa kazi kubwakubwa na Rais Ruto. Huo sio msingi dhabiti wa kutuhimiza tupinge maandamano,” akasema katibu wa muungano huo Bw Kelvin Macharia.

Bw Macharia alisema kwamba “njia ya kipekee kuhakikisha tunaunga mkono serikali ya Rais Ruto kikamilifu ni kupitia kutupa raha ya kufurahia jasho letu ambalo alituahidi angetekeleza iwapo tungemchagua”.

Sasa, Bw Macharia akiongea mjini Murang’a alisema “sisi tulimchagua Bw Ruto pasipo shinikizo na matumaini yetu yalikuwa angetimiza aliyotuahidi”.

Alisema kwamba “kwa sasa kile tunashuhudia ni wale waliopewa kazi wakizurura Mlima Kenya wakitoa matusi kwa vyombo vya habari, kwa viongozi wenzao na kwa Wakenya wenzao walio katika upinzani”.

Bw Macharia alisema kwamba waliopewa kazi na Ruto hawasinywi na gharama kuu ya maisha na ndio sababu hawaelewi ubutu wao wa kimaongezi unakera wananchi.

Bw Macharia alimtaka Bw Gachagua kuelewa jinsi ya kuongea, ambapo badala ya kujigamba vile wengi wamepewa kazi serikalini, aanze kuelezea ni manufaa gani serikali hiyo imeletea wapiga kura wa Mlima Kenya.

“Ukitwambia tulinde serikali hii ya hisa, unapaswa utuelezee mgao wetu wa faida kama wapiga kura ni gani, uko wapi na utaingia mifukoni mwetu lini,” akasema.

Bw Macharia aliteta kwamba “hawa viongozi wetu wana mazoea ya kuhadaa wapiga kura…Wale wa upinzani wakitumiwa vibaya kuandamana, sisi tunatumiwa vibaya kuunga serikali mkono tunayoambiwa ni yetu pasipo manufaa yoyote”.

Bw Macharia alisema kwamba “wakulima wa Mlima Kenya hawajali iwapo serikali ya Ruto itasambaratishwa na upinzani ikiwa haijitumi kuwapa pesa mfukoni kama ilivyowaahidi”.

Alisema kwamba “kinachoweza kusababisha tukosane na upinzani ni ikiwa mgao wetu wa faida katika serikali hii ya hisa unakuja kama tulivyoahidiwa lakini ikiwa sababu tunayopewa ni kwamba Gachagua na wenzake wamepewa kazi, basi acha njia ya muongo iwe fupi”.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Vibarua wa kiume walalamikia mabroka wa bidhaa za mashamba...

Panya wamejaa katika hospitali za Kaunti ya Murang’a –...

T L