• Nairobi
  • Last Updated June 1st, 2024 3:21 PM
Viongozi Pwani kufanya kazi na Rais Ruto bila miegemeo ya kisiasa kwa ajili ya maendeleo

Viongozi Pwani kufanya kazi na Rais Ruto bila miegemeo ya kisiasa kwa ajili ya maendeleo

NA CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa kisiasa wa pwani hatimaye wameamua kuungana na kufanya mazungumzo na Rais William Ruto kuhusu namna eneo hilo litafaidi kimaendeleo chini ya utawala huu wa Kenya Kwanza.

Wakiongozwa na Spika wa Seneti Amason Kingi, viongozi hao walisema Alhamisi kwamba watajadiliana na Rais kuhusu namna eneo hilo litafaidi kutokana na mpango wa serikali wa kukodisha huduma mbalimbali katika bandari ya Mombasa na Lamu kwa sekta ya kibinafsi.

Waliwatwika Bw Kingi na mawaziri Aisha Jumwa (Jinsia) na Salim Mvurya (Madini) wajibu wa kufanya mazungumzo na Dkt Ruto kuhusu masuala ya kimaendeleo waliyokubaliana katika mkutano huo katika mkahawa wa Serena, Nairobi.

“Leo (Alhamisi) tumekutana kama viongozi wa pwani ili tubaini yale tunaweza kufanya ili eneo letu lifaidi kimaendeleo katika serikali hii iliyoko mamlakani ndani ya miaka mitano. Mkutano wa leo uliwaleta pamoja wabunge, maseneta, magavana, mawaziri, maspika wa mabunge yote sita ya pwani, magavana wa zamani miongoni mwa wengine, bila kujali miegemeo yao ya kisiasa,” Bw Kingi akasema baada ya mkutano huo uliodumu kwa zaidi ya saa nne.

Alifafanua kuwa siasa hazikujadiliwa katika mkutano huo wa kwanza wa aina yake wa viongozi wa pwani kutoka mirengo na vyama mbalimbali vya kisiasa.

Akisoma maamuzi yaliyoafikiwa katika mkutano huo, Gavana wa zamani wa Mombasa Ali Hassan Joho alikariri kujitolea kwa viongozi wa pwani kufanyakazi pamoja kwa manufaa ya wakazi wa eneo hilo.

“Kama viongozi wa pwani, bila kujali vyama vyetu vya kisiasa, tumeamua kuungana kwa misingi ya ajenda ya maendeleo ya eneo letu,” akasema.

“Pili tumeamua kuwa viongozi wa kaunti zote sita za pwani wataratibu masuala muhimu ya maendeleo ambayo tutawasilisha mbele ya Rais wa Jamhuri ya Kenya. Mazungumzo yatahusu jinsi ya kuchochea maendeleo yanayoendeleza masilahi ya watu wetu,” akaongeza Bw Joho ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa chama cha ODM.

Hata hivyo, gavana huyo wa zamani alisema kuwa mkutano huo ulikubaliana kuhusu masuala ya dharura na ambayo “yanapasa kushughulikiwa wakati huu.”

“Tumeamua kumfikia Rais William Ruto kujadilia suala nyeti la ubinafsishaji au ukodishaji wa bandari ya Mombasa, bandari ya Lamu, bandari ya Shimoni na bandari yoyote ile ambayo itajengwa pwani siku zijazo,” Bw Joho akaeleza.

Mwanasiasa huyo alisema waliamua kulipa kipaumbele suala la bandari ya bandari hizo “kwa sababu kama wakazi wa pwani kitega uchumi chetu na chumi za kaunti zetu zinategemea pakubwa shughuli za bandari.”

Bw Joho pia alitangaza kuwa viongozi hao wa pwani watakutana tena katika kaunti ya Lamu mwezi ujao kupiga msasa ajenda za maendeleo ambazo watakuwa wakiamua zishughulikiwe ndani ya miaka mitano ya utawala wa Rais Ruto.

“Ni baada ya hapo ambapo tunaweza kuzungumzia masuala ya siasa kwa sababu lengo letu kama viongozi ni kuboresha maisha ya watu wetu,” akaeleza.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni mawaziri; Aisha Jumwa na Salim Mvurya, magavana Abdulswamad Nassir (Mombasa), Gideon Mung’aro (Kilifi), Fatuma Achani (Kwale), wabunge, maseneta na maspika wa mabunge ya kaunti.

Viongozi wa pwani wamekuwa wakipinga vikali mpango wa serikali wa ubinafsishaji wa bandari za Mombasa na Lamu wakisema mpango huo utawakosesha nafasi ya kufaidi kutokana na rasilimali hizo.

Ni baada ya presha za viongozi hao ambapo mnamo Septemba 29, 2023, Rais Ruto alijitokeza na kufafanua kuwa serikali yake haitabinafsisha bandari hizo.

Akiongeza wakati wa mkutano wa Baraza la Kitaifa la Uongozi wa chama cha UDA,  katika Bomas of Kenya, Rais Ruto alisema badala yake serikali yake itakodisha baadhi ya huduma za bandari hizo kwa sekta ya kibinafsi.

  • Tags

You can share this post!

Karen Nyamu atishia kuchochea wanawake Nairobi kuvua nguo...

Mwanamume aliyekiri kuiba mkate na maziwa Naivas kuhukumiwa...

T L