• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wakazi wa Manda-Maweni watabasamu shirika likitoa chakula na matibabu ya bure kwa wanyama

Wakazi wa Manda-Maweni watabasamu shirika likitoa chakula na matibabu ya bure kwa wanyama

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa kisiwa cha Manda-Maweni katika Kaunti ya Lamu wamejitokeza kupokea chakula cha msaada cha wanyama na pia matibabu ya bure ya wanyama hao wakati ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Wanyama Duniani.

Hafla hiyo iliongozwa na Kituo cha Matibabu ya Punda (Donkey Sanctuary), tawi la Lamu kwa ushirikiano na maafisa wa Idara ya Mifugo ya Kaunti ya Lamu.

Wanyama waliopokea matibabu hayo ya bure na chakula ni punda, mbuzi na mbwa.

Matibabu yalijumuisha usafishaji na kuziba vidonda, chanjo, na ukaguzi wa afya ya wanyama hao.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku hiyo muhimu, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Matibabu ya Punda nchini Dkt Solomon Onyango, aliwahimiza wananchi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha haki za wanyama zinalindwa.

Dkt Onyango alisisitiza haja ya wenye wanyama kuwapa upendo, chakula, matibabu ya mara kwa mara na pia kuhakikisha wanalala vizuri.

Wakazi wa Manda-Maweni wapokea chakula cha kulisha wanyama wanaofuga. PICHA | KALUME KAZUNGU

Aliwashauri wakazi pia kuzingatia usafi wa mazingira ambapo wanyama wanaishi.

Akigusia punda, Dkt Onyango alisisitiza haja ya wanyama hao kupewa muda wa kutosha wa kupumzika na wamiliki kuepuka kuwatesa kupitia kuwapiga, kuwabebesha mizigo mizito isiyo ya kiwango chao.

“Leo tukiadhimisha Siku ya Wanyama Duniani, ninawasihi wananchi kuwa mstari wa mbele kuepuka ukaidi wa haki za wanyama. Wanyama wana hisia kama sisi na hawastahili kuteswa. Siridhiki nikiona mtu akimtesa mnyama kama punda licha ya manufaa aliyo nayo kijamii na hata kiuchumi. Tumtunze punda atutunze. Pia tuzingatia kuwatunza vyema Wanyama wengine,iwe Ni mbuzi, ng’ombe, kuku, ngamia, paka na kadhalika,” akasema Dkt Onyango.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Afisa Mkuu Msimamizi wa Idara ya Mifugo, Kaunti ya Lamu, Bw Sharif Kamalu alisema karibu wanyama 80,000 kote Lamu tayari wamepokezwa chanjo ya kudhibiti maradhi, yakiwemo yale ya mapafu.

Baadhi ya wanyama waliopokezwa chanjo hiyo kote Lamu ni ng’ombe zaidi ya 45,000, mbuzi 25,000, mbwa 4,200 na punda 2,700.

Wakazi wa Manda-Maweni katika Kaunti ya Lamu wajitokeza kunufaika na matibabu ya bure kwa wanyama huku pia wakipewa lishe ya bure kwa wanyama hao wakati wa kuadhimisha Siku ya Wanyama Duniani katika kituo cha Matibabu ya Punda kinachofahamika kama Donkey Sanctuary. PICHA | KALUME KAZUNGU

Alisema zoezi hilo bado linaendelea maeneo tofauti ya Lamu, akiwahimiza wenye wanyama kujitokeza kupokezea chanjo kuzuia msambao wa maradhi ya wanyama eneo hilo.

“Wakati tukiadhimisha Siku ya Wanyama Duniani, ningeomba sana wananchi kuzingatia kuongeza mapenzi kwa viumbe hawa. Si makosa kumpenda punda au paka kiasi cha kumkaribisha mezani kwako mle pamoja mlo. Tukiwatunza hawa wanyama watatufaidi sana,” akasema Bw Kamalu.

Kwa upande wake, Afisa wa Matibabu ya Mifugo Kaunti ya Lamu Felix Rachuonyo aliwasihi wananchi kutumia siku hiyo kuwapumzisha wanyama wao na hata kuhakikisha wanawawasilisha kwa kituo cha Matibabu ya Punda kisiwani Lamu na washirika wengine ili waangaliwe hali zao za afya.

“Kama Idara ya Mifugo, tunashirikiana na wadau wote wakiwemo hawa wa hii Donkey Sanctuary katika kutoa huduma za mifugo eneo hili. Najua kuna wale wanaodharau wanyama. Watambue kuwa haki za Wanyama lazima ziheshimiwe. Tumejitolea kutibu wanyama bure leo na huu ndio wakati wa wananchi kuchukua fursa kuwawasilisha wanyama wao ili wafaidi haya matibabu ya bure na ushauri pia,” akasema Bw Rachuonyo.

Mmoja wa wakazi wa Manda-Maweni aliyenufaika na msaada huo wa chakula na matibabu ya bure kwa wanyama, Bi Lilian Okoth, aliwapongeza wadau kwa kuzingatia kuadhimisha Siku ya Wanyama Duniani hapo kijijini kwao.

“Sisi kazi zetu zote hapa ambazo nyingi zinahusisha kubeba mizigo mizito ya mawe ya kujengea tunazifanya kutumia punda. Tumefurahi kwa msaada tuliopata leo,” akasema Bi Okoth.

Kauli yake iliungwa mkono na mmiliki wa punda, Bw Justus Mwaniki, aliyewashauri wakazi wenzake kuzingatia kukimu wanyama wao vilivyo kimaslahi, ikiwemo kuwapa matibabu na chakula.

“Kituo cha Donkey Sanctuary leo kimetuonyesha mfano mwema wa jinsi wanyama wetu wanavyofaa kutunzwa. Pia tumepokea ushauri na tutazingatia yote wakati tunapotumia hawa wanyama kwa njia moja au nyingine. Wenzangu pia nawashauri tuige mfano tulioonyeshwa leo,” akasema Bw Mwaniki.

  • Tags

You can share this post!

Mwamko mpya Roam ikifungua nchini Kenya kiwanda cha...

Katuni, Oktoba 4, 2023

T L