• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Wakenya 3 wateuliwa kujiunga na muungano wa madaktari ulimwenguni

Wakenya 3 wateuliwa kujiunga na muungano wa madaktari ulimwenguni

NA PAULINE ONGAJI

WAKENYA watatu wameteuliwa kama washauri rasmi katika Baraza la Muungano wa Madaktari ulimwenguni (WMA).

Madaktari hao ambao ni wanachama wa muungano wa madaktari nchini KMA, waliteuliwa katika uteuzi uliofanyika katika kikao cha baraza la WMA cha 223 kinachoendelea jijini Nairobi kati ya Aprili 20 na Aprili 22.

Walioteuliwa ni pamoja na Dkt Diana Marion atakayewakilisha KMA katika kamati ya uadilifu ya WMA na Dkt Lyndah Kemunto ambaye atakuwa katika kamati ya fedha na mipango.

Kwa upande mwingine, Dkt Brenda Obondo atawakilisha muungano huo katika kamati ya maslahi ya kijamii.

Huku akihutubia wanachama wa WMA kutoka mataifa mbalimbali katika jumba la kimataifa la mikutano KICC, Rais wa WMA, Dkt Osahon Enabulele, alionyesha wasiwasi kuhusu uhaba wa uwekezaji katika sekta ya afya, vilevile mazingira duni ya kufanya kazi miongoni mwa madaktari na wahudumu wengine wa kiafya hasa barani Afrika.

“Na hivyo tungependa kuhimiza serikali ya Kenya, vilevile uongozi wa mataifa mengine ya Afrika kuwekeza vilivyo katika sekta ya afya.”

Maoni yake yaliungwa mkono na Rais wa KMA, Dkt Simon Kigondu, KMA, aliyesisitiza umuhimu wa kuongeza idadi ya madaktari nchini, kuambatana na kiwango cha wagonjwa.

Muungano wa WMA ni shirikisho la kimataifa linalowakilisha madaktai milioni tisa ulimwenguni kote.

Kwa upande mwingine, KMA ni mwanachama wa WMA ambapo imekuwa ikitetea ubora wa huduma za afya nchini, vile vile afya na maslahi ya madaktari.

  • Tags

You can share this post!

Kiraitu Murungi arejea serikalini

Wanabodaboda: Hatutashiriki maandamano ya Azimio

T L