• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:50 AM
Wakenya washauriwa wawe waangalifu machafuko yakishuhudiwa Ethiopia

Wakenya washauriwa wawe waangalifu machafuko yakishuhudiwa Ethiopia

Na CHARLES WASONGA

IDARA ya Polisi imewataka Wakenya kuchukua tahadhari za kiusalama kufuatia machafuko yanayoshuhudiwa nchini Ethiopia.

Vita vilivyokithiri haswa katika jimbo la Tigray kati ya waasi na wanajeshi wa serikali vilichangia serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutangaza hali ya hatari nchini humo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano, msemaji wa Polisi Bruno Shioso alisema kuwa serikali imetambua kuwa vita vinavyoendelea katika taifa hilo na mataifa mengine jirani vinaweza kuvuruga amani.

Bw Shioso alieleza kuwa mapigano katika mataifa hayo haswa yanaweza kuhujumu amani katika maeneo yanayopakana na mataifa kando na raia wa mataifa hayo kuingia nchini.

“Kama jirani wa Ethiopia na baadhi ya mataifa yanayoathirika na machafuko, Kenya inaweza kuathirika vibaya na matukio yatakayotokana na mapigano hayo,” taarifa hiyo ikasema.

“Kwa sababu hii, idara ya polisi inawataka Wakenya kuwa waangalifu katika maeneo yanakoishi haswa mipakani,” ikaongeza.

Bw Shioso alitoa wito kwa wananchi kutoa ahabari kwa kituo cha karibu cha polisi endapo watawaona wageni au wahamiaji wanaowashuku.

Msemaji huyo wa polisi alisema doria za usalama zimeimarishwa kote nchini haswa katika maeneo ya mipaka na katika na vituo mbalimbali vya kiusalama nchini.

You can share this post!

Ruto aahidi yaliyoshinda UhuRuto

Benzema afunga mabao mawili na kusaidia Real...

T L