• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 AM
Wandayi: Tutavuruga usomaji bajeti

Wandayi: Tutavuruga usomaji bajeti

Na GEORGE ODIWUOR

WABUNGE Wa upinzani wametishia kuvuruga usomaji wa bajeti iwapo Mswada wa Fedha wa 2023 utapitishwa bungeni bila kufanyiwa marekebisho.

Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi alisema kuwa kama wabunge wa upinzani, watazua vurugu kuhakikisha kuwa Waziri wa Fedha Profesa Njuguna Ndung’u hasomi bajeti iwapo masuala ambayo wameyaibua sasa hayatashughulikiwa.

Bw Wandayi aliongeza kuwa wabunge wote wa ODM wameamrishwa wapinge mswada huo unaokabiliwa na utata wakati ambapo utawasilishwa kujadiliwa bungeni baadaye mwezi huu, Juni 2023.

Hata hivyo, iwapo utapitishwa na kupisha kusomwa kwa bajeti, wabunge wa upinzani watahakikisha wametumia njia nyingine kuhakikisha bajeti yenyewe haisomwi kwa sababu utaumiza Wakenya.

“Wakenya wengi wamekataa mswada huu. Sioni kwa nini bunge linastahili kuupitisha,” akasema Bw Wandayi.

“Iwapo utapitishwa, tuhakikisha kuwa waziri wa fedha hasomi bajeti. Hakuna haja ya mtu yeyote afike bungeni kusoma bajeti ambayo haizingatii maslahi ya Wakenya,” akasema mbunge huyo.

Wakenya wengi wamekuwa wakipinga mswada huo hasa kutokana na pendekezo tata la kuwatoza asilimia tatu kwenye mshahara wao, pesa ambazo zitaelekezwa katika hazina ya nyumba.

Pia mswada huo unapendekeza kuongezwa kwa ushuru wa mafuta kutoka asilimia nane ya sasa hadi asilimia 16.

Kinara wa upinzani Raila Odinga na viongozi wengine wamekuwa wakipinga mswada huo na hata kutishia kuongoza maandamano makubwa iwapo utapitishwa.

Bw Wandayi alisema hayo baada ya kuungana na baadhi ya wabunge wa ODM kwenye mkutano wa kisiasa katika eneobunge la Kasipul, Kaunti ya Homa Bay.

Mbunge huyo anayehudumu muhula wake wa tatu, alipendekeza kuwa mswada huo unafaa kurejeshwa kwa kamati ya bajeti ya bunge kisha ufanyiwe marekebisho kabla ya kurejeshwa kwa wabunge kuujadili.

“Mswada huo tayari una matatizo na utakuwa kupoteza wakati kuujadili bungeni ilhali ni bayana Wakenya hawautaki,” akasema Bw Wandayi.

Mwanasiasa huyo alilalamika kuwa juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na upinzani kuboresha maisha ya Wakenya hazijakuwa zikizaa matunda, kwa hivyo kilichosalia ni kuvuruga usomaji wa bajeti.

Baadhi ya wabunge ambao waliandamana na Bw Wandayi ni TJ Kajwang’ (Ruaraka), Adipo Okuome (Karachuonyo), Lillian Gogo (Rongo) na Rosa Buyu wa Kisumu Mjini Magharibi.

Bw Wandayi pamoja na wabunge wenzake pia waliwashtumu baadhi ya wabunge wa ODM ambao wamehamia mrengo wa serikali na sasa wanafanya kazi na Rais William Ruto.

Wabunge hao ni Gideon Ochanda (Bondo), Caroli Omondi (Suba Kusini), Elisha Odhiambo (Gem), Mark Nyamita (Uriri), Felix Odiwuor (Lang’ata), Paul Abuor (Rongo) na Walter Owino (Awendo).

Bw Were alimshutumu Rais William Ruto kwa kuwahadaa Wakenya kuwa atashughulikia changamoto zinazowakabili kama kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi.

“Rais Ruto ni mwongo. Amekuwa akisema ataimarisha maisha ya Wakenya ilhali mambo yanazidi kuwa magumu,” akasema Bw Were.

  • Tags

You can share this post!

Akothee na mumewe, fungate yapamba moto

Babu Owino: Wakenya wakombolewe kutoka kwa minyororo ya...

T L