• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Watakaopigwa darubini kali 2022

Watakaopigwa darubini kali 2022

Na WAANDISHI WETU

KATIKA mwaka huu wa 2022, macho ya Wakenya yatawalenga baadhi ya watu wanaoshikilia nyadhifa muhimu kwa kuamua mwelekeo wa kisiasa, uchaguzi mkuu, haki na uchumi.

Bw Wafula Chebukati

Kama mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Chebukati pia ni afisa mkuu msimamizi mkuu wa uchaguzi wa urais.

Katika majukumu hayo yote, macho yote ya Wakenya yataelekezwa kwake anapoongoza tume hiyo katika kusimamia uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati. PICHA | MAKTABA

Rais mpya atachaguliwa wakati wa uchaguzi huo, sawa na magavana, maseneta, wabunge na madiwani.

Bw Chebukati ametoa hakikisho kwamba IEBC itasimamia uchaguzi huo kwa njia huru na haki.

Jaji Mkuu Martha Koome

Jaji mkuu Bi Koome ni sharti ahusishwe katika masuala ya uchaguzi mkuu.

Katika mwaka huu wa uchaguzi, Jaji Mkuu anasimamia majaji wa Mahakama ya Juu kusikiza kesi cha kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais, ilivyofanyika katika chaguzi za 2013 na 2017.

Jaji Mkuu Martha Koome. PICHA | MAKTABA

Kando na masuala ya uchaguzi wa urais, Bi Koome na majaji wa mahakama ya juu wakati huu wanasikiza kesi kuhusu hatima ya mswada wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI). Kesi kadha ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu pia huenda zikafika katika mahakama ya juu.

Mutahi Kagwe

Huku janga la Covid-19 ikiendelea kuwa tisho kikuu la kiafya katika duniani, haswa nchini Kenya, waziri wa afya atakuwa na wajibu mkubwa katika utekelezaji wa mikakati ya kupambana na janga hilo nchini.

Pia ataongoza kampeni za kuvumisha mpango wa utoaji chanjo ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa corona.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ahutubia taifa kuhusu hali ya janga la kiafya la Covid-19 mwishoni mwa mwaka 2021. PICHA | MAKTABA

Kuhusu iwapo nchi itafungwa kufuatia kupanda kwa visa vya maambukizi ya aina mpya ya kirusi cha corona kwa jina Omicron, kutategemea utendakazi wa Bw Kagwe. Kutategemea ushauri ambao Bw Kagwe na maafisa wake watatoa kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Kagwe pia atategemewa pakubwa katika utekelezaji wa Mpango wa Afya kwa Wote (UHC). Mpango huo utatekelezwa kwa usaidizi wa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF). Asasi hiyo inaongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji Peter Kamunyo.

Dkt Patrick Njoroge

Huku biashara mbalimbali na uchumi kwa ujumla ukiendelea kuathirika na Covid-19 na thamani ya shilingi ya Kenya ikipungua, Benki Kuu ya Kenya (CBK) itachangia pakubwa katika ukarabati wa uchumi.

Yule ambaye atafanya maamuzi kuhusu ukarabati wa uchumi sio mwingine ila Gavana wa CBK Patrick Njoroge.

Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Dkt Patrick Njoroge. PICHA | SALATON NJAU

Gavana huyo pia atakuwa mstari wa mbele katika utayarishaji wa kanuni za kusimamia shughuli za mashirika yanayotoa mikopo kwa njia dijitali.

Ezra Chiloba

Miezi mitatu baada ya kuteuliwa kwake kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (CA), Bw Ezra Chiloba tayari ametisha kufutilia mbali leseni na masafa ya jumla ya redio 60 kwa kufeli kutimiza masharti ya leseni hizo.

Kabla ya hapo, Bw Chiloba alipiga marufuku runinga ya Sasa TV inayomilikiwa na Pasta James Ng’ang’a wa Kanisa la Neno Evangelism.

Afisa huyo alichukua hatua hiyo kwa sababu ilipeperusha vipindi vyenye maudhui chafu.

Bw Chiloba pia atatekeleza wajibu mkubwa katika upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Hii ni kwa sababu mamlaka ya CA ndio husimamia mawimbi ya mawasiliano.

Prof George Magoha

Mwaka huu mpya ni muhimu katika mchakato mzima wa utekelezaji wa mtaala mpya wa umilisi na utendaji (CBC) utakaoongozwa na Waziri Profesa Magoha.

Vile vile, waziri huyo anaanza mwaka na wajibu mkubwa wa kufanikisha ujenzi wa madarasa 10,000 yatakayotumika na wanafunzi wa gredi 5 watakaojiunga na kiwango cha kwanza cha shule za upili katika mwaka wa 2023.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha. PICHA | MAKTABA

Mitihani ya KCPE na KCSE itakayofanyika mwaka huu 2022 pia itatoa nafasi kwa kurejelewa kwa kalenda ya kawaida ya masomo iliyovurugwa na janga la Covid-19.

You can share this post!

Hali ngumu kuandama Wakenya 2022

Mapinduzi yalivyotishia demokrasia Afrika 2021

T L