• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Washukiwa 11 wafumaniwa wakikata magari ya serikali

Washukiwa 11 wafumaniwa wakikata magari ya serikali

NA SAMMY KIMATU

MAKACHERO katika kituo cha polisi cha Industrial Area wamewakamata washukiwa 11 waliopatikana katika gereji moja wakiwa katika kukurukakara za kukatakata magari ya serikali.

Aidha, miongoni mwa magari yaliyopatikana yakiharibiwa ni pamoja na malori manne, gari moja aina ya pick-up na lori la idara ya zimamoto linalomilikiwa na serikali ya kaunti ya Nairobi.

Vyuma vilivyokatwa kutoka kwa gari la idara ya zimamoto. PICHA | SAMMY KIMATU

Naibu kamanda wa polisi Makadara, Bw Dennis Omuko alisema uhalifu huo ulifanyika katika yadi moja mkabala wa barabara ya Dakar, Eneo la Viwanda.

Bw Omuko aliongeza kwamba nia ya washukiwa ilikuwa ni kuuza vipande vya magari hayo kwa wafanyabiashara wa vyuma chakavu.

Naibu kamanda wa polisi Makadara, Bw Dennis Omuko. PICHA | SAMMY KIMATU

Aliongeza kwamba washukiwa wamezuiliwa katika kituo cha Industrial Area wanakohojiwa kabla ya kupelekwa katika mahakama ya Makadara.

“Tunafuatilia kisa hiki kwa makini zaidi kwa sababu kuna uhusiano na watu fulani kutoka kwa serikali kuu sawia na serikali ya kaunti,” Bw Omuko akasema.

Polisi walikokota malori manne na kuyazuilia katika kituo cha polisi cha Industrial Area.

Katika kituo cha Industrial Area, tulipata lori moja likiwa limejaa vipande vya vyuma vilivyokuwa tayari vimekatwa.

Kando yake, Bw Omuko alionyesha wanahabari vyuma vilivyopatikana baada ya gari la idara ya zimamoto kuharibiwa.

Bw Omuko pia aliwashukuru wananchi kwa kujitolea kuwadokezea polisi habari kuhusu uhalifu huo.

  • Tags

You can share this post!

Ulawiti: Papa Francis asema viongozi wa kidini wahitaji...

Mtalii Shella hatakiwi kunywa pombe, kuvaa minisketi...

T L