• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 2:35 PM
Waziri Bore ashikilia makao binafsi kuokoa watoto sharti yafungwe

Waziri Bore ashikilia makao binafsi kuokoa watoto sharti yafungwe

NA JESSE CHANGE

WAZIRI wa Leba na Masuala ya Kijamii, Florence Bore amesisitiza kuhusu mpango wa serikali kufunga vituo vya kibinafsi kutunza watoto.

Waziri Bore amesema hatua hiyo inatokana na ongezeko la visa vya ulanguzi wa watoto nchini, serikali ikitoa makataa ya miaka 10 kwa wanaomiliki makao ya kibinafsi kuyafunga.

Tayari, miaka miwili imeisha tangu tangazo hilo litolewe na Bi Bore anasema serikali itatumia vituo vyake kulinda watoto wanaotelekezwa.

Waziri alitoa himizo hilo alipozuru Shirika la Kuangazia Maslahi ya Watoto Nchini, tawi la Kanduyi, Kaunti ya Bungoma.

“Nimekuja leo kuhakikisha ustawi wa watoto wanaoishi chini ya ulinzi wa tawi la Bungoma. Ni jukumu letu kulinda watoto wa taifa letu,” akasema Waziri Bore.

Alitetea maamuzi ya serikali, akisema hatua hiyo inalenga kuhakikishia usalama wa watoto.

Waziri wa Leba na Masuala ya Kijamii, Florence Bore alipozuru mojawapo ya makao kuokoa watoto Bungoma. PICHA|JESSE CHENGE

Alisisitiza kwamba ni jukumu la serikali kuhakikisha kwamba kila mtoto anaishi katika mazingira

“Kila mtoto anastahili kuwa katika mazingira salama. Tutatoa makazi ya muda wakati juhudi za kuwaunganisha tena na familia zao au malezi mbadala zinaendelezwa,” alifafanua.

Aidha, aliahidi kuwa serikali itaweka mipango maalum makao ya watoto kote nchini.

“Tayari tumeanza ujenzi wa miundombinu mpya ili kukidhi mahitaji ya watoto zaidi. Upangaji huu unalenga kutoa mazingira salama na yenye upendo,” alisema.

Ongezeko la kutisha la kesi za kutelekezwa kwa watoto katika eneo la Magharibi limezua wasiwasi mkubwa.

Wakati wa ziara yake, Waziri alihimiza wazazi na walezi kuchukua jukumu kwa ustawi wa watoto wao.

Waziri Bore amekuwa akizuru vituo mbalimbali nchini vya kulea watoto walioachwa, mayatima na hata waliotelekezwa kwa lengo la kubaini usalama wa mazingira wanayoishi.

 

[email protected]

 

 

  • Tags

You can share this post!

Akothee adai kuwa mjamzito baada ya kuachana na mumewe...

Ken Lusaka alalamikia siasa za kaunti kutishia utendakazi...

T L