• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
Waziri Kuria: Tutapeleka maandamano kwa Kenyatta

Waziri Kuria: Tutapeleka maandamano kwa Kenyatta

Na MERCY KOSKEI

WASHIRIKA wa Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya wakiongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua wamefichua mipango ya kufanya mkutano wa maandamano nje ya makaazi ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Kiambu.

Hatua hiyo inalenga kupinga kurejea kwa Kenyatta katika ulingo wa kisiasa, wakisema taswira ya majuzi kuzuru afisi za Jubilee ni ishara kutaka kudhibiti chama.

“Tutafanya mkutano huo si popote pengine ila nje ya nyumba ya familia ya Kenyatta katika kijiji cha Ichaweri, Gatundu Kusini, Kiambu.Iinaweza ikawa wiki hii,” alisema Waziri wa Biashara Moses Kuria.

Akizungumza siku ya Jumapili katika uwanja wa Thika, wakati wa kuadhimisha ya miaka 25 msanii Muigai Wa Njoroge kwenye uimbaji, Waziri huyo alisema kuwa lazima wamfunze Kenyatta kuwa wao ndio wenye mamlaka.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua kama mgeni wa heshima, ambapo alimpa Wa Njoroge kima cha Sh2 milioni mchango wake na wa Rais William Ruto.

Wengine waliohudhuria na kuunga mkono maoni ya Bw Kuria ni gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi, mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, mwakilishi wa wanawake Kiambu Anne wa Muratha, Mbunge wa Thika mjini Alice Ng’ang’a na Seneta wa Kiambu Karungo Thang’wa.

Bw Kuria alimshutumu Kenyatta, akidai anakula njama za kisiasa kuvuruga serikali ya Rais Ruto na vile vile “kutatiza uwekezaji kupitia kufadhili misukosuko inayochochewa na upinzani”.

Akizungumzia kuhusu Raila Odinga, Bw Kuria alidai kuwa anaongoza maandamano dhidi ya serikali, akisema kuwa “kuna watu ambao Bw Kenyatta anaunga mkono ambao wanajulikana kwa kupigana uwekezaji kupitia maandamano.”

“Jamii yetu haijulikani kupigania vitega uchumi vya watu na ndivyo Bw Kenyatta anafanya…Hilo ndilo tutakalomwambia katika mkutano huo nje ya boma lake,” alisema Kuria

Bw Gachagua alimkashifu Kenyatta na aliyekuwa Katibu Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho, kwa kile alidai walikuwa makuhani wa pombe haramu eneo la Kati.

“Siku ya Alhamisi, nitakutana na wawakilishi wadi, maspika na maseneta pamoja na wale wanatambua sheria ili watuunge mkono kupigana na pombe haramu Mlima Kenya,” alisema.

Aliongeza kuwa kuna wale wanaolenga kuzima jitihada zake kukomboa ngome yake kutoka kwenye kinywa cha pombe haramu na hatari.

Aliahidi kuendelea kutetea masuala ya Mlima Kenya.

Bw Gachagua alisema tayari wabunge wa eneo la Mlima Kenya wamearifiwa kuanza kutunga sheria ya kura moja mtu mmoja, ili kuelekeza maendeleo kwa wakazi wengi wa eneo hilo.

 

  • Tags

You can share this post!

Upasuaji wa miili 10 ya wahanga Shakahola waonyesha...

Kivumbi leo Azimio wakiapa kuingiza wafuasi katikati mwa...

T L