• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Wito wa kujiamini barani Afrika, kujitafutia suluhu ya matatizo watawala kongamano la Kusi Ideas

Wito wa kujiamini barani Afrika, kujitafutia suluhu ya matatizo watawala kongamano la Kusi Ideas

STEVE OTIENO NA CHARLES WASONGA

MAKALA ya tano ya Kongamano la Kuzuzuana Mawazo la KUSI Ideas Festival limeanza huku viongozi wa Afrika wakitakiwa kuwa wabunifu, wenye bidii na kujitolea kusukuma ajenda ya maendeleo ya bara hili kufikia 2063.

Mkutano huo unaendelea jijini Gaborone nchini Bostwana na umewaleta pamoja wajumbe kutoka nchi kadha za Afrika, wakiwemo marais, wakuu wa sekta mbalimbali, watungaji sera, wajasiriamali, wadau katika majukwaa ya kidijitali na wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu.

Wajumbe wanaohudhuria kongamano hilo kimtandao na kibinafsi wanatarajiwa kuibua mawazo yanayotarajiwa kutoa suluhu kwa changamoto zinazokumba bara Afrika.

Akitoa hotuba yake ya ufunguzi, Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi alilinganisha kongamano hilo na soko la hisa ambapo watu wanakutana kubadilishana mawazo yanayoweza kuleta manufaa.

Aidha, alilitaja kama jukwaa la kutoa sera ambazo zinaweza kuzalisha mapato kwa manufaa ya nchi za Afrika.

Mkutano huo, Rais Masisi alisema, ilipatia wadau muhimu nafasi ya kukadiria kiwango cha kujitolea kwao kutekeleza mpango wa kimaendeleo kwa Afrika na hivyo kuimarisha uwezo wa mataifa ya bara hili kufikia malengo ya Ajenda ya Maendeleo ya 2063.

“Tumeshawishika kikamilifu kwamba mkutano huu unatoa nafasi kwa viongozi kutoka bara Afrika kuchanganua masuala mbalimbali na kuweka juhudi zetu za pamoja,” akasema.

Rais Masisi aliongeza kuwa mada zitakazojadiliwa na wakuu wa serikali, sekta za kibinafsi, mashirika ya kijamii, wawekezaji na asasi mbalimbaili zitachangia maono ya pamoja ya kimaendeleo ya Afrika.

Muhimu katika ufikiaji wa malengo hitajika itakuwa ni Afrika iliyoungana na inayoenda mbele kwa lengo moja huku ikiimarisha juhudi zake za kuendeleza ushirikiano wa kibiashara.

“Ni nafasi yetu ya kutafakari kuhusu mianya ya ufanisi na changamoto kwa mipango ya maendeleo Afrika. Bila shaka sote tunachangamkia Mkataba wa Biashara Huru Kati ya Mataifa ya Afrika (ACFTA) ulioanza kutekelezwa 2021.

Rais huyo wa Bostwana alionya wajumbe dhidi ya kudhani kuwa mwaka wa 2063 ni mbali akisema zimesalia miaka 40 kuufikia.

“Watu wengi hapa ni wenye umri mdogo na wanashikilia nyadhifa za uongozi. Hii ndio maana mkutano huu unatoa jukwaa kwa watu kama hao kuratibu mustakabali wanaoutaka,” Bw Masisi akasema.

Miongoni mwa masuala muhimu yanayojadiliwa katika kongamano la mwaka huu ni pamoja na kuligeuza bara la Afrika kuwa lenye ufanisi, linaloongozwa na mkataba wa kibiashara unaofanyakazi, uzingativu wa sheria na haki za kibinadamu na kuendelezwa kwa utawala bora na demokrasia. Aidha, kongamano hilo linajadili umuhimu wa kuwepo kwa amani Afrika na kuungwa mkono mwa juhudi za Umoja wa Afrika (AU) kurejesha amani katika nchi zinazokumbwa na vita.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirika la Habari la Nation (NMG) Dkt Wilfred Kiboro aliwataka Waafrika kujipa moyo kwamba wanao uwezo wa kuleta ufanisi katika bara hili.

Alishangaa ni vipi watu wengi Ulaya, sehemu za bara Asia na Amerika wangali wanadhani Afrika ni nchi moja ilhali ina mataifa mengi.

“Hii ina maana kuwa Afrika haijajinadi ipasavyo ulimwenguni,” akasema.

Dkt Kiboro pia alisema Afrika inapasa kuwajibikia maendeleo yake na ikome kutizama enzi za ukoloni ambapo Waafrika walitendewa aina mbalimbali za unyama na watawala wa kigeni.

“Naamini kuwa hatupasi kuendelea kulaumu nchini zilizotutawala kwa madhila yanayokumba Afrika. Nashawishika kuwa tuko na uwezo wa kukabiliana na changamoto zote zinazotukumba na kupata masuluhisho ya kutufaa.

Mojawapo ya suala kuu ambalo ningetaka tujadili katika kongamano hili ni jinsi ya kuondoa fikra za kikoloni mawazoni mwetu ni tujiamini kama Waafrika wenye suluhu kwa changamoto zinazotukumba,” akasema.

Shirika la NMG ni mwandalizi mwenza wa kongamano hilo.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa aliwahimiza viongozi wa Afrika kuungana kwa lengo la kuwahudumia raia wao na wakome kufurahisha viongozi wa nchi zilizoendelea.

“Kama Afrika twapaswa kuzungumza kwa sauti moja. Sharti tutambuliwe kama viongozi wazuri kwa watu wetu na tukome kujipendekeza au kufurahisha vingozi wa nchi za Magharibi,” akasema.

Wengine waliohutubu ni Waziri Mkuu wa Rwanda Edouard Ngirente na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa.

  • Tags

You can share this post!

Demu wa beste yangu ataka tupige mechi ya kisiri ugenini

Aliuza mbuzi wake kupata pesa za Krismasi, lakini jambazi...

T L