• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Aliuza mbuzi wake kupata pesa za Krismasi, lakini jambazi akamvamia usiku, akamwibia na kumuua

Aliuza mbuzi wake kupata pesa za Krismasi, lakini jambazi akamvamia usiku, akamwibia na kumuua

NA MWANGI MUIRURI

Mwanamume wa miaka 57 kutoka Kaunti ya Murang’a aliyekuwa ameuza mbuzi wake kwa Sh12, 000 za kufadhili sherehe za msimu wa Krismasi amenyang’anywa hela hizo na kuuawa.

James Kamau kutoka Kijiji cha Kigoro katika eneo bunge la Maragua alikuwa ameuza mbuzi huyo Desemba 5, 2023 katika soko na akarejea nyumbani kupanga bajeti yake.

“Lakini usiku mwendo wa saa sita alivamiwa na jambazi aliyekuwa amebeba shoka na petroli na akamkata kichwani akimdai hela hizo,” akasema Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini Bw Gitonga Murungi.

Bw Murungi alisema kwamba ripoti zilizokusanywa kutoka kwa mashahidi zinaashiria kwamba jambazi huyo wa kiume alikuwa na ripoti tosha kuhusu kuwepo kwa pesa hizo katika boma la Kamau.

“Jambazi huyo akiwa peke yake aliingia katika boma hilo lakini hakuwa akijua vyema nyumba hasa ya Kamau. Alivunja nyumba ya Bi Naomi Nyambura na baada ya kumhangaisha akimwitisha pesa, na kugundua alikuwa kwa nyumba tofauti na aliyokuwa analenga, akatoka,” akasema Bw Murungi.

Aliongeza kwamba jambazi huyo akitoka na akavunja mlango wa nyumba ya Kamau na ambapo alizua fujo kuu akiitisha pesa.

Naibu Kamishna wa Maragua Joshua Okello aliambia Taifa Leo kwamba “wa kwanza kukutana na jambazi huyo alikuwa ni mke wa Kamau kwa jina Jane Waruguru.

“Bi Waruguru aligongwa kichwani akiulizwa alikokuwa mumewe pamoja na pesa. Bibi alijitolea kuelezea zilikokuwa pesa kwa kibeti ndani ya nyumba,” akasema Bw Okello.

Jambazi huyo aliyeelezewa na mashahidi kuwa mnene na aliyekuwa akitumia lugha ya Kiswahili alielekea katika nyumba ya malazi alikoelezewa pesa ziko na akakumbana na Kamau aliyekuwa akienda kujua kilichomfanya mkewe kupiga nduru pamoja na vurugu ndani ya nyumba.

“Kamau aligongwa kichwani na akapoteza fahamu huku jambazi huyo akihepa na pesa na simu mbili. Kizazaa hicho kilichukua takribani dakika 25,” akasema Bw Okello.

Bw Murungi alisema kwamba Kamau aliaga dunia katika hospitali ya Murang’a baada ya kuvunja damu kupindukia.

“Naye Bi Waruguru alikimbizwa hadi hospitali ya Thika ambako amelazwa akiwa na majeraha kichwani. Msako dhidi ya jambazi huyo umezinduliwa na tunaomba wananchi watusaidie kumnasa,” akasema.

Wenyeji walilamika kwamba visa vya mvamizi huyo dhidi ya boma za eneo hilo vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara huku wakuu wa kiusalama mara mbili wakitangaza kunaswa kwake lakini hatimaye kuibuka ilikuwa propaganda tu ya serikali.

“Kwa kipindi cha miezi minne sasa jambazi huyo amevamia maboma 15 na kuua watu wanne. Wakuu wa kiusalama wa kaunti wametangaza kukamatwa kwa mshukiwa huyo lakini hata wakati tunatarajia awe korokoroni, anatuvamia na kutuua. Kwani huwa wanamwachilia atuvamie na kisha anarejea kwa kituo cha polisi?” akahoji Bi Mary Njuguna, mkazi wa Kabuta.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wito wa kujiamini barani Afrika, kujitafutia suluhu ya...

Mamia wafutwa kazi katika kiwanda cha kahawa mikakati ya...

T L