• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Yesu Wa Tongaren: Kwangu polisi walipata sadaka ya Sh225, nyanya na vitunguu

Yesu Wa Tongaren: Kwangu polisi walipata sadaka ya Sh225, nyanya na vitunguu

NA SAMMY WAWERU

IMEBAINIKA askari walipata Sh225 nyumbani kwa Mhubiri Eliud Simiyu almaarufu Yesu Wa Tongaren.

Alipowapeleka makachero wa Idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) katika boma lake Kijiji cha Lukhokhwe, Bungoma, Mei 13, 2023 mchungaji huyo amesema pia walipata nyanya na vitunguu.

Yesu Wa Tongaren alitoa ufichuzi huo Jumanne, Mei 16, 2023 baada ya mahakama Bungoma kuamuru aachiliwe huru.

“Mbali na sadaka ya Sh225, pia walipata nyanya na vitunguu,” alisema.

Mtumishi huyo wa Mungu ambaye ni mwasisi wa Kanisa la New Jerusalem, alieleza kutoridhishwa kwake na hatua ya askari kumkamata licha ya kushirikiana nao kufanya uchunguzi.

Afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (ODPP) iliagiza korti kuachilia huru Yesu Wa Tongaren, ikisema ushahidi uliowasilishwa na DCI hauna msingi wowote kumfungulia mashtaka.

Bw Simiyu alitiwa pingu Mei 10, 2023 kwa tuhuma za kupotosha waumini wake.

Isitoshe, polisi walidai anaandamwa na mashtaka ya biashara haramu ya pesa na kupokea fedha za uhalifu.

Wakenya mitandaoni walijitokeza kumtetea, wengi wakihoji ni mhubiri mcheshi ambaye baada ya kutathmini utendakazi wake hawaoni makosa yake wala sababu za kukamatwa.

Mapema 2023 alipohojiwa na Taifa Leo, alidai kwamba ni jumla ya watu 168, 000 pekee kote duniani watakaoenda mbinguni.

Kilichozua ucheshi zaidi, alidai kwamba Nairobi ni watu wawili pekee watakaouona Ufalme wa Mungu na isitoshe hawajazaliwa.

Msimu wa Pasaka 2023, alienda mafichoni japo alijitokeza baadaye baadhi ya wakazi Bungoma walipotishia kumsulubisha sawa na Yesu Mwana wa Mungu.

Simiyu, hata hivyo, alidai tayari ameshasulubiwa, na kwamba hawezi kusulubishwa kwa mara ya pili.

 

 

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Polisi wachunguza kifo cha raia usalama ukidorora

Ajali ya tuktuk na lori yasababisha vifo vya watatu Kilifi

T L