• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Polisi wachunguza kifo cha raia usalama ukidorora

Polisi wachunguza kifo cha raia usalama ukidorora

NA SIAGO CECE

POLISI mjini Diani wanachunguza kifo cha raia mmoja aliyetoweka na kupatikana kichakani.

Mkazi wa mji wa Showground Ukunda Bw Meshak Owaka mwenye umri wa miaka 56 aliripotiwa kutoweka mnamo Mei 6, 2023 na mwili wake kupatikana Jumanne katika kichaka .

Lakini polisi katika afisi ya Msambweni walihakikisha kuwa mwili uliopatikana kichakani karibu na bahari ulikuwa wake, baada ya raia kutangaza kuwa wameona mtu kichakani.

Afisa Mkuu wa Polisi Kaunti Ndogo ya Msambweni Bw Francis Gachoki alisema kuwa bado wanachunguza chanzo cha kifo chake.

“Tumeangalia mwili na tumehakikisha kuwa ni yeye. Bado hatujabaini ni nini kilichomuua. Uchunguzi unaendelea,” Bw Gachoki alisema.

Haya yanajiri huku wakazi wa Diani na Ukunda wakizua hofu kutokana na ongezeko la visa vya uhalifu mjini huo.

“Kila kona kuna vijana ambao wanaibia wakazi na hii ni wasiwasi mkubwa kwetu. Kuna wengine wanatembea na kutisha watu na bunduki,” Sara Ochieng, mkaazi moja alisema.

Aliomba polisi kuongeza kupiga doria katika mitaa yote ili kukabiliana na visa hivyo vinavyoendelea kuongezeka hasa usiku.

Hapo awali wakazi wamekuwa wakilalamika kuibiwa simu na pesa wakitembea barabarani usiku.

Visa chache vya wizi wa pikipiki pia vimeripotiwa na muungano wa bodaboda kaunti hiyo.

“Hatuelewi ni nini kinaendelea. Tumepoteza takriban pikipiki saba chini ya wiki moja,” Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda Kwale Nehemiah Kinyua alisema.

Aliwaomba polisi wabidiike kukabiliana na visa vya uhalifu eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

Yesu Wa Tongaren sasa ni huru kusafisha dhambi za Wakenya

Yesu Wa Tongaren: Kwangu polisi walipata sadaka ya Sh225,...

T L