• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
100 wafa, maelfu wapoteza makao katika janga la mafuriko nchini Sudan

100 wafa, maelfu wapoteza makao katika janga la mafuriko nchini Sudan

NA MASHIRIKA

KHARTOUM, SUDAN

ZAIDI ya watu 100 wameuawa na maelfu ya wengine kuachwa bila makao kutokana na mafurika yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoshuhudiwa nchini Sudan.

Kufuatia janga hilo serikali ilitangaza hali ya hatari katika mikoa sita nchini humo iliyoathirika zaidi.

Afisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa ya Kushirikisha Utoaji Misaada ya Kibinadamu Alhamisi jioni ilisema kuwa jumla ya watu 258,000 wameathirika na mafuriko katika mikoa 15 kati ya 18 nchini Sudan.

Mashirika ya habari yaliripotiwa kuwa wakazi wengi wamelazimika kuondoka makwao tangu mvua ilipoanza kunyesha majuma mawili yaliyopita.

Gezira ni moja ya majimbo ambako serikali imetangaza mafuriko kuwa janga la kitaifa. Vijiji kadha vimezama tangu msimu wa mvua ulipoanza hali ambayo imewaacha mamia ya familia bila makazi.

Waathiriwa wengi wametafuta hifadhi mpya katika maeneo kavu katika nyanda za juu.

Hata hivyo, wanalalamika kuwa hawajapata usaidizi kutoka kwa serikali, mashirika ya kutoa msaada na wahisani wengine.

“Tuliamka na kupata maji yakiwa yametapakaa katika nyumba zetu na tukaondoa yale ambayo tuliweza kuokoa. Kila mara sisi husikia kuwa nyumba imeporomoka au mfumo wa utoaji maji taka umepasuka au ukuta umeanguka. Hakuna kilichosalia,” Adam Ismail, mkazi wa eneo la Wad Alnaeim, aliambia shirika la habari la Al Jazeera.

Ismail aliongeza kuwa amekuwa akisubiri maji yapungue ili yeye na mamake warejee kijijini kujenga nyumba yao upya.

Lakini wiki mbili baadaye, raia huyo hajui atasubiri hadi lini kwa sababu hakuna dalili kwamba maji yatapungua.

“Msimu wa mvua umetajwa kama mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Sudan kwani mvua imeathiri sehemu zote nchini humo,” mwanahabari mmoja akasema.

  • Tags

You can share this post!

Karan Patel na Jasmeet Chana wanafufua uadui Nanyuki Rally

TAHARIRI: Klabu za Ligi Kuu zijishughulishe vilivyo msimu...

T L