• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
AU yapanga kupunguza idadi ya wanajeshi wake Somalia

AU yapanga kupunguza idadi ya wanajeshi wake Somalia

Na JULIUS BARIGABA

ADDIS ABABA, Ethiopia

UMOJA wa Afrika (AU) umetangaza kuwa utapunguza idadi ya wanajeshi wake wa kulinda amani nchini Somalia (AMISOM) ndani ya miaka mitano ijayo, kutokana na kupungua kwa ufadhili.

Hii ni baada ya kukamilika kwa muhula wa kuhudumu wa kikosi cha sasa, mwishoni mwa mwaka huu wa 2021.

Duru zilisema kuwa kufikia sasa Serikali ya Somalia na wafadhili wakuu wamekubaliana na mpango huo wa kupunguzwa kwa wanajeshi wa Amisom.

Wataalamu wa masuala ya amani na usalama katika AU wanafanya ukadiriaji wa mahitaji makuu ya wanajeshi na maafisa wasaidizi, yatakayowezesha kufanikishwa kwa mpango huo.

“Ukadiriaji huo ndio utawezesha kujulikana kwa mahitaji ya kifedha, silaha na vifaa vinginevyo vya kivita ili ijulikane kiasi cha fedha kitakachohitajika kwa mpango,” akasema afisa mmoja wa AMISOM ambaye aliomba jina lake libanwe.

Kulingana na ripoti ya kikosi cha AU kilichoendesha ukadiriaji, wajibu wa kimsingi wa kikosi hicho kipya utakuwa ni kupiga jeki Jeshi la Somalia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kiusalama.

Jeshi la Somalia pia litapokea mafunzo zaidi ili kuimarisha uwezo wake, chini ya mpango huo wa AMISOM.

Hata hivyo, mwezi jana, raia mmoja wa Somalia Harun Maruf, alisema kuwa wakati umetimu kwa AMISOM kusitisha kabisa shughuli zake nchini humo.

Alisema licha ya kikosi hicho kuwa nchini Somalia kwa miaka 14 hakijaafikia mengi ilivyotarajiwa kwani wafuasi wa al-Shabaab wangali wanatekeleza mashambulio kila mara nchini humo.

Mkosoaji mwingine anasema kuongezwa kwa muda wa shughuli za AMISOM kwa zaidi ya mwaka mmoja “kutaleta madhara mengine kando na kupoteza rasilimali.”

Umoja wa Mataifa (UN), wataalamu wa masuala ya usalama na mataifa yanayochangia wanajeshi hata hivyo yanaelezea hofu ya al-Shabaab kuvuruga Mogadishu tena AMISOM ikiondoka kabisa nchini Somalia.

Vile vile, kuna wasiwasi kwamba miji mingine ya Somalia pia itavamiwa na kudhibitiwa na wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi lenye uhusiano na al-Qaeda.

Ripoti moja iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pia linaibua hofu kwamba usalama utazorota nchini Somalia baada ya kuondolewa kwa wanajeshi wa Amerika ambao wamekuwa wakitekeleza mashambulio ya angani katika vituo vya al-Shabaab.

Ripoti hiyo pia inasema kuwa shughuli za AMISOM zimelisaidia jeshi la Somalia kudhibiti Al Shabaab kama miji na vijiji ambavyo awali vilitekwa na kundi hilo la kigaidi.

  • Tags

You can share this post!

Leicester City wazamisha chombo cha Norwich ligini

Uwanja wa ndege kujengwa eneo la Gatuanyaga