• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Biden kuzuru mpaka wa Ukraine na Poland

Biden kuzuru mpaka wa Ukraine na Poland

NA AFP

WASHINGTON D.C., AMERIKA

RAIS Joe Biden anatarajiwa kutembelea mpaka wa Poland na Ukraine huku serikali ya Amerika ikisema kuwa, haiungi mkono wito wa kutaka kiongozi wa Urusi Vladimir Putin auawe.

Rais Biden atatua mjini Rzeszow, Poland kilomita 80 kutoka mpaka wa Ukraine.

Ziara hiyo ya Biden inaashiria kuwa Amerika iko tayari kupambana na majeshi ya Urusi iwapo yatathubutu kurusha makombora nchini Poland.

Nchini Poland, Rais Biden atakutana na wanajeshi wa Amerika wa kikosi cha 82nd Airborne Division waliotumwa nchini humo kwa lengo la kuilinda kutokana na hofu kwamba huenda ikashambuliwa na Urusi.

Poland ni mwanachama wa Muungano wa Majeshi ya Ulaya na Amerika (NATO).

Jana Ijumaa, Ikulu ya White House ilipuuzilia mbali wito wa Seneta wa Amerika aliyetaka Rais Putin auawe.

“Huo sio msimamo wa serikali ya Amerika na bila shaka siyo tamko utalisikia kutoka kinywani mwa yeyote anayefanya kazi na serikali ya Rais Biden,” alisema Jen Psaki, msemaji wa White House.

Seneta Lindsey Graham wa chama cha Repulican kutoka South Carolina, katika mahojiano na kituo cha Fox News, alimtaka mtu mmoja nchini Urusi kujitoa mhanga na kumuua Putin.

“Ili kumaliza uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, mtu mmoja nchini Urusi lazima asimame na kumuondoa jamaa huyu (Putin),” alisema seneta huyo.

Wakati huo huo, Mkuu wa mashitaka katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) Karim Khan jana Ijumaa alielezea wasiwasi wake kutokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Khan alisema ataanzisha uchunguzi wa uhalifu wa kibinadamu dhidi ya Urusi.

Ukraine iliitaka ICC kuchunguza Urusi baada ya kuipokonya jimbo la Crimea mnamo Machi 2014 kufuatia mapigano kati ya taifa hilo na waasi walioungwa na Urusi.

Jana Ijumaa, milipuko na milio ya risasi ilikuwa ikisikika katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, wakati majeshi ya Urusi na Ukraine yalikuwa yakipigania udhibiti wa mji huo.

Serikali ya Ukraine imetangaza amri ya kutotoka nje kati ya saa kumi na moja jioni mpaka saa mbili asubuhi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alitabiri kuwa mapigano mjini Kyiv yataongezeka zaidi leo Jumamosi.

“Hatuwezi kuupoteza mji mkuu wa nchi yetu – tutapigana hadi mwisho,” Rais Zelenskyy alisema kupitia mtandao wa Twitter.

Alisema kuwa, silaha na vifaa vya kivita kutoka kwa washirika wa Ukraine viko njiani kuelekea Kyiv.

Amerika ilidai Ijumaa kuwa asilimia 60 ya makombora yanayorushwa na wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine yamekuwa yakifeli.

Kwa mujibu wa Amerika, wanajeshi wa Urusi wamerusha angalau makombora 1,100 tangu vita hivyo kuanza Februari 2022, lakini mengi yalifeli.

  • Tags

You can share this post!

Gavana Twaha apuuzilia mbali EACC kuhusu ripoti ya ufisadi

Kuria aagizwa kufika mbele ya kamati ya IEBC

T L