• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
Tanzania yakana mpango wa kufungia raia makwao kuepuka corona

Tanzania yakana mpango wa kufungia raia makwao kuepuka corona

Na MASHIRIKA

SERIKALI imesema kuwa Watanzania wanaotaka kujifungia nyumbani kwa hiari kuepuka maambukizi ya virusi vya corona wako huru kufanya hivyo huku kukiwa na hofu kuhusu ongezeko la kasi ya maambukizi ya maradhi hayo nchini humo.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt Hassan Abbas aliwataka Watanzania kutokuwa na hofu huku akisema Rais John Pombe Magufuli hana mpango wa kufungia Watanzania nyumbani.

“Watanzania hawatafungiwa ndani; shughuli ziendelee kama kawaida zile za burudani, michezo, ofisini na mashambani ziendelee na inapobidi watu wachukue tahadhari.

“Lakini wewe ukiona hutaki kutoka nje jifungie mwenyewe lakini msimamo wa serikali haitafungia watu au kuzuia shughuli za kiuchumi,” amesema Dkt Abbas ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari.

Msemaji wa serikali aliyekuwa akizungumza jijini Dodoma alitoa msimamo, baada ya chama cha upinzani cha ACT- Wazalendo kutangaza kuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad pamoja na mkewe wanaugua ugonjwa wa corona.

Chama cha ACT Wazalendo Jumapili kilisema kuwa, aliyekuwa mwaniaji wake wa urais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad ambaye sasa ni makamu wa kwanza wa rais, anaendelea kupata afueni. Baadhi ya walinzi wake pia walipatikana na virusi vya corona.

Chama hicho cha upinzani sasa kimeitaka serikali kuweka mikakati itakayowezesha Watanzania kuzingatia kanuni za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza kuwa virusi vya corona vimeisha nchini Tanzania. Lakini wiki iliyopita, kiongozi huyo alisema kuwa: “Kuna watu walienda kuchanjwa Corona katika mataifa ya kigeni na wametuletea corona ya ajabu ajabu.”

Wakati huo huo, Chama cha Mawakili nchini Tanzania (TLS) pia kimeelezea hofu yake baada ya wanachama wake 10 kufariki kutokana na maradhi yasiyojulikana ndani ya miezi miwili iliyopita.

TLS kilisema Jumapili kuwa hii ni mara ya kwanza kwa chama hicho kupoteza idadi kubwa ya wanachama wake ndani ya miezi miwili.

Ibada katika makanisa Jumapili zilitawaliwa na ujumbe wa kuwataka waumini kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza alisema uhai ni mali binafsi, si mali ya kanisa wala Serikali.

You can share this post!

Bobi Wine afika mahakamani kupinga ushindi wa Museveni

Kansa ya lango la uzazi bado changamoto mashambani