• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Bobi Wine azimwa kuelekea Amerika kwa kutotimiza masharti ya kudhibiti Covid-19

Bobi Wine azimwa kuelekea Amerika kwa kutotimiza masharti ya kudhibiti Covid-19

Na DAILY MONITOR

KIONGOZI wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi Sentamu, maarufu kama Bobi Wine, Ijumaa alizuiwa kusafiri hadi Amerika kwa kutotimiza masharti ya corona.

Mwanasiasa huyo ambaye ni rais wa chama cha National Unity Platform (NUP) alitarajiwa kuhudhuria kongamano la Uganda Action Day and Convention alipoarifiwa kuwa hangeweza kusafiri.

Hii ni kwa sababu kulingana na kanuni iliyowekwa na taifa la Amerika, mtu ambaye amewahi kuwa nchini Afrika Kusini sharti akae nchini mwake kwa siku 14 kwanza kabla ya kusafiri kuelekea nchini.

“Niliambiwa kuwa Amerika imeweka sheria kwamba ikiwa ulikuwa Afrika Kusini, huwezi kuingia humo kabla ya siku 14 kutamatika. Ni juzi tu ambapo nilikuwa Afrika Kusini na hivyo singeweza kuruhusiwa kuenda Amerika,” Bobi Wine akawaambia wanahabari katika afisi za chama cha NUP katika kitongoji cha Kamwokya, jijini Kampala.

“Nitafuatiliwa shughuli za kangamano hilo kwa njia ya mtandao, kutoka Uganda,” mwanasiasa huyo ambaye pia ni mwanamuziki akaongeza.

Safari ya Bobi Wine, ambaye aliwania urais mwaka 2020 na kushikilia nambari mbili katika uchaguzi uliodaiwa kujaa udanganyifu, ya kuenda Amerika ilitibuka jijini Doha, Qatar.

“Sikufahamu kuhusu marufuku hayo mapema. Maafisa mjini Entebbe pia hawakuwa na habari kuhusu vikwazo hivi na hivyo hawakunishauri. Kwa sababu hiyo ilinilazimu kurejea Uganda,” akaeleza.

Hata hivyo, viongozi wengine wa NUP akiwemo Mbunge Francis Zaake na Mwenyekiti Nyanzi waliruhusiwa kuendelea na safari na sasa watamwakilisha Bobi Wine katika mkutano huo.

“Naomba radhi zaidi kwa wale waliotarajia uwepo wangu mimi binafsi katika kongamano hilo na shughuli nyinginezo,” Bobi Wine akasema.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Shirika la kutafutia wakulima soko lawahimiza kukuza mimea...

Aston Villa wapiga Man-United breki kali ligini